• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
NYOTA WA WIKI: Rafael Leao

NYOTA WA WIKI: Rafael Leao

NA GEOFFREY ANENE

NYOTA Rafael Leao aliibuka mchezaji wa wiki ya 28 kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu wa 2022-2023 ambao umeingia mkondo wa lala salama.

Alipata mafanikio hayo baada ya kuongoza AC Milan kubomoa wenyeji Napoli 4-0 ugani Diego Armando Maradona mjini Naples, hapo Aprili 2.
Raia huyo wa Ureno alitetemesha nyavu za viongozi Napoli mara mbili.

Ana mabao 10 kabla ya mchuano dhidi ya Lecce hapo Aprili 7, idadi inayomfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Milan kufikisha magoli 10 misimu miwili mfululizo, tangu Mwitaliano Mario Balotelli msimu 2013-2014.

Leao ni kati ya watoto sita – wanaojumuisha wasichana wawili pacha – wa wazazi wanaotokea barani Afrika nchini Angola na Sao Tome & Principe.
Jina lake Leao kwa Kireno linamaanisha moyo wa simba, alilopewa baada ya kuzaliwa.

Leao anafahamika kwa chenga zake, kufyatuka na mpira na weledi wa kukamilisha mashambulizi.

Amelinganishwa kimchezo na Mfaransa Kylian Mbappe, Mbrazil Neymar, Mkorea Son Heung-min, Mbrazil Gabriel Martinelli na hata Muingereza Marcus Rashford miongoni mwa wengine.

Thamani yake sokoni (Sh10.2 bilioni) inamweka nyuma ya mawinga matata duniani Mreno Bernardo Silva kutoka Manchester City (Sh11.1 bilioni) na Mbrazil Rodrygo anayechezea Real Madrid (Sh10.6 bilioni).

Iko mbele ya mastaa kama raia wa Uruguay Federico Valverde kutoka Real Madrid (Sh9.6 bilioni), Mmisri Mohamed Salah wa Liverpool (Sh9.5 bilioni) na Neymar (Sh9.0 bilioni).

Leao, ambaye pia ni mbunifu, anatumia miguu yote, ingawa mguu wake wa kulia ni hatari zaidi.

Kimataifa, Leao amechezea Ureno tangu timu ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 16.

Aliingia timu ya watu wazima mnamo Oktoba 2021 chini ya kocha Fernando Santos na kufikia sasa ameisakatia michuano 18.

Amefunga mabao matatu na kusuka pasi nne zilizojazwa kimiani.

Leao alikuwa katika kikosi cha Ureno kilichosalimu amri ya Morocco 1-0 katika robo-fainali ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Anamezewa mate na Real Madrid, Chelsea na Manchester United, ingawa pia inasemekana waajiri wake Milan wanataka kuongeza kandarasi yake itakayokatika 2024.

  • Tags

You can share this post!

Ni Pasaka ya sala na msoto

Wapenzi wa Kiswahili wamuenzi Walibora, familia ikililia...

T L