• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Oleksandr Zinchenko sasa mali rasmi ya Arsenal

Oleksandr Zinchenko sasa mali rasmi ya Arsenal

Na MASHIRIKA

ARSENAL wamekamilisha uhamisho wa Oleksandr Zinchenko, 25, kutoka Manchester City kwa Sh4.3 bilioni.

Sogora huyo raia wa Ukraine ametia saini mkataba wa miaka minne ugani Emirates na ni mchezaji wa tano kujiunga na Arsenal muhula huu baada ya Matt Turner, Marquinhos, Fabio Vieira na Gabriel Jesus.

Anakuwa nyota wa pili kutokea Man-City na kuingia katika sajili rasmi ya Arsenal muhula huu baada ya Jesus aliyetua Emirates kwa Sh6.7 bilioni mwezi uliopita.

“Hatimaye ndoto yangu ya tangu utotoni ya kujiunga na Arsenal imetimia. Nilianza kutazama mechi za Arsenal kikosi hicho kilipokuwa kikijivunia huduma za Thierry Henry na Cesc Fabregas,” akasema Zinchenko.

Ingawa amekuwa akiwajibishwa na Ukraine kama kiungo, Zinchenko alikuwa beki wa kushoto kambini mwa Man-City. Alichezea miamba hao mara 15 mnamo 2021-22 na akasaidia kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kuhifadhi ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza.

“Nimezungumza na kocha Mikel Arteta wa Arsenal kuhusu majukumu yangu kikosini na nitakuwa radhi kuwajibishwa katika nafasi yoyote atakayoitaka,” akaelezea Zinchenko.

“Niko hapa kujikuza kitaaluma na kuongoza Arsenal kushinda mataji. Tutapigania ubingwa wa makombe ya vipute vyote tutakavyokuwa tukishiriki,” akaongeza.

Chini ya Arteta, Arsenal wanapania kutumia zaidi ya Sh20 bilioni kujisuka upya muhula huu na wanatazamiwa kutwaa kiungo mahiri raia wa Ubelgiji, Youri Tielemans, kutoka Leicester City kadri wanavyolenga kurejea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu 2017.

“Zinchenko ni mchezaji wa haiba mwenye uwezo wa kuwajibishwa katika nafasi mbalimbali kikosini. Analeta tajriba pevu na ubunifu mkubwa. Tutarajie mambo makuu zaidi kutoka kwake,” akasema Arteta aliyewahi kumnoa Zinchenko ugani Etihad alipokuwa mkufunzi msaidizi wa Man-City.

Zinchenko alikuwa miongoni mwa wanasoka wa kwanza kusajiliwa na Guardiola kambini mwa Man-City mnamo 2016 baada ya kuagana na FC Ufa ya Urusi.

Tangu wakati huo, Man-City wamemwajibisha mara 128 katika mashindano yote na akaongoza kikosi hicho kutia kapuni Kombe la FA, ubingwa wa League Cup mara nne na mataji manne ya EPL.

Wakati uo huo, Arsenal wamefichua mpango wa kurefusha mkataba wa kiungo Bukayo Saka, 20, ili kuwapiga kumbo Man-City wanaomvizia chipukizi huyo katika juhudi za kujaza pengo la Raheem Sterling aliyeyoyomea Chelsea.

Kwa mujibu wa Arteta, Saka atakuwa sasa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa mshahara wa juu zaidi ugani Emirates ikizingatiwa kuwa ujira wake wa sasa wa Sh10 milioni kwa wiki utaongezeka maradufu. Thomas Partey na Jesus ndio wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi kambini mwa Arsenal. Kila mmoja wao hutia mfukoni Sh29 milioni kwa wiki.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ndege ya kwanza yapeleka miraa baada ya mkataba wa marais

Apu zinazoongoza wakulima na wafugaji katika shughuli zao

T L