• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Apu zinazoongoza wakulima na wafugaji katika shughuli zao

Apu zinazoongoza wakulima na wafugaji katika shughuli zao

NA SAMMY WAWERU

ATHARI za tabianchi zinaendelea kubadilisha mkondo wa hali ya hewa, ukame, mkurupuko wa magonjwa ya mimea na wadudu vyote vikihangaisha shughuli za kilimo na ufugaji.

Misimu ya mvua imesambaratika, kero ambayo imesababishia baadhi ya wakulima hasara mimea na mazao kucharazwa na kiangazi na mifugo kufa njaa.

Hali hiyo ikizidi kulemea Kenya, Somalia na Ethiopia, katika Upembe wa Afrika, wadau sekta ya kilimo na ufugaji, watafiti na Wanasayansi wanasisitiza haja kukumbatia mifumo ya teknolojia za kisasa.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro) imebuni apu ya simu inayosaidia wakulima kujua mvua itakaposhuhudiwa.

Shirika hilo la kiserikali, pia limezindua apu nyingine inayotoa maelekezo ya hali ya hewa katika eneo, mimea inayopaswa kukuzwa ikiwa ni pamoja na shughuli za ufugaji bora.

Kenya Agricultural Observatory Platform (Kaop), kwa kutumia simu tamba za kisasa inapatikana kwenye safu ya playstore.

Mkulima akishaiweka kwenye simu yake kupitia muongozo ataweza kutambua hali ya hewa kwa muda wa siku 15 zijazo.

“Inamrahisishia kujua hali ya hewa ilivyo katika mazingira yake, ili kupanga shughuli za upanzi,” asema Judy Wambugu, mtaalamu ICT kutoka taasisi hiyo.

Apu hiyo, mkulima anafuatilia maelezo akiwa alipo yanayojumuisha mvua na kiwango cha joto.

Judy anaambia Akilimali kwamba Kalro imekumbatia tabiri za setilaiti, na kushirikisha kaunti zote 47.

Apu hiyo ya kidijitali inaenda sambamba na Kalro Crop Selector.

Mtaalamu wa ICT shirika la Kalro, Judy Wambugu akionyesha utendakazi wa apu ya kidijitali Kalro Crop Selector inayoelekeza mkulima kujua mimea bora ya kukuza katika mazingira yake. PICHA | SAMMY WAWERU

Selector, nayo inawezesha mkulima kujua aina ya mimea anayopaswa kukuza katika mazingira yake, kupitia mahitaji ya hali ya hewa.

Isitoshe, inashauri mifugo bora katika eneo pamoja na malisho faafu kukuza.

Mkulima mtumizi, akishaingia mtandaoni achague kaunti aliyoko, kisha kaunti ndogo na hatimaye wadi kupata maelezo anayosaka.

Katika wadi, ukurasa wa maelezo na mashauri nasaha yanajitokeza Judy akisema Kalro ina wataalamu wanaohudumia mitambo mfululizo, saa 24, kupokea maombi ya wanaopiga simu wakitaka msaada.

“Kila saa wako ange kushauri wakulima na wafugaji,” aelezea, akisema apu hizo hazitozwi malipo.

Ada iliyoko ni mkulima anapopigia wataalamu simu, kupitia nambari zilizotolewa.

Anadokeza kwamba, shirika hilo lina zaidi ya apu 35 zinatoa ushauri nasaha wa kilimo bora na faafu kuanzia upanzi hadi mavuno.

Mbali na rununu, mkulima anaweza kujiandikisha kupata huduma za apu hizo kupitia tovuti yazo.

Mapokezi ya mfumo huo wa kidijitali yanazidi kunoga, idadi ya waliojisajili ikigonga milioni 1.3.

“Mambo mengi yanaenda kidijitali, na mifumo tuliyozindua ni kati ya teknolojia zinazosaidia wakulima kupata ushauri nasaha wa kilimo bora,” Judy asema.

Huku Kalro ikisaidia kuboresha kilimo na ufugaji nchini, wadau katika sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) wamehimiza kampuni na mashirika yanayotoa huduma za intaneti nchini kushusha gharama.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya ICT, Dkt Paul Kipronoh amesema malengo ya Kenya kuimarisha sekta hii kupitia dijitali huenda yakalemezwa na bei ya juu ya data na huduma za intaneti.

“Gharama ya intaneti mashambani ni ghali mno, na ni maeneo yaliyosheheni vijana wanaofanya kilimo na ufugaji.

“Tunapoendeleza mjadala kuboresha sekta hii ambayo ni nguzo kuu ya uchumi nchini, tutathmini bei ya huduma za intaneti,” Dkt Kipronoh ahimiza.

 

  • Tags

You can share this post!

Oleksandr Zinchenko sasa mali rasmi ya Arsenal

IEBC: Ruto ataka Rais azime polisi

T L