• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Olunga nje ya Kombe la Dunia la Klabu

Olunga nje ya Kombe la Dunia la Klabu

Na GEOFFREY ANENE

Mabingwa wa Qatar, Al Duhail, ambao wameajiri Mkenya Michael Olunga walibanduliwa Alhamisi kwenye Kombe la Dunia la Klabu linaloendelea mjini Al Rayyan. Al Duhail walipoteza mchuano wa robo-fainali 1-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika na Misri Al Ahly.

Mshambuliaji matata Olunga, ambaye allibuka mchezaji bora na mfungaji bora Japan mwaka 2020, alichezeshwa kipindi cha kwanza pekee kabla ya kupumzishwa na kocha Sabri Lamouchi na nafasi yake kutwaliwa na mshambuliaji mzawa wa Ghana Mohammed Muntari ambaye ni raia wa Qatar.

Lamouchi, ambaye ana asili ya Tunisia, alifanya mabadiliko mawili kabla ya kipindi cha pili kuanza. Aliingiza mshambuliaji mzawa wa Sudan raia wa Qatar Almoez Ali, ambaye allibuka mchezaji bora na pia mfungaji bora kwenye Kombe la Bara Asia mwaka 2019, katika nafasi ya beki Bassam.

Al Duhail ilifanya badiliko tena dakika ya 72 wakati Ismail Muhammad alichukua nafasi ya Ahmed Yasser kabla ya kuingiza Louise Martin dakika 10 baadaye kuchukua nafasi ya Ali Karimi.

Mabadiliko hayo yote hayakuweza kuokoa wenyeji hao kutokana na bao ambalo Hussein El Shehat alifunga Al Duhail dakika ya 30. Refa aliongeza dakika sita za majeruhi, lakini pia hazikutosha kuepushia washiriki wapya kabisa Al Duhail kipigo hicho.

Al Ahly sasa itamenyana na miamba wa Bara Ulaya na Ujerumani Bayern Munich katika nusu-fainali hapo Februari 7. Nusu-fainali nyingine itakuwa kati ya Tigres UANL kutoka Mexico na Wabrazil Palmeiras. Mabingwa wa Amerika ya Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) Tigres walijikatia tiketi baada ya kutoka nyuma na kuzaba washindi wa Bara Asia Ulsan Hyundai kutoka Korea Kusini 2-1 katika robo-fainali ya kwanza Februari 4.

Mfaransa Andre-Pierre Gignac alifungia washiriki wapya kabisa Tigres mabao yote, moja ikiwa penalti. Kama tu Bayern, wafalme wa Copa Libertadores (Amerika ya Kusini) Palmeiras walijikatia tiketi ya nusu-fainali moja kwa moja kwa kushinda ubingwa wa eneo lao. Fainali ni Februari 11.

You can share this post!

Man-City wacharaza Burnley tena na kujiweka pazuri kutwaa...

Mwanasiasa adai kutekwa na kutupwa msituni