• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Omanyala kupimana ubabe na Mwamerika Bracy jijini Zagreb

Omanyala kupimana ubabe na Mwamerika Bracy jijini Zagreb

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala atafufua uhasama dhidi ya Mwamerika Marvin Bracy-Williams mjini Zagreb, Croatia kwenye riadha za makumbusho ya Borisa Hanzekovica, Jumapili.

Omanyala, ambaye ni bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola, alilemewa na Bracy kwa nukta 0.01 katika mashindano ya Spitzen Leichtathletik Luzern nchini Uswisi mnamo Agosti 29. Afisa huyo wa polisi aliandikisha 10.18 naye Bracy 10.17 huku raia wa Jamaica Ackeem Blake akifunga tatu-bora kwa 10.22 katika mashindano hayo ya kwanza ya Omanyala tangu atawazwe bingwa wa Jumuiya ya Madola mjini Birmingham, Uingereza mnamo Agosti 3.

“Sina presha. Matarajio yangu ni kushinda,” alisema Omanyala aliyepanga kusafiri hadi Zagreb mnamo Septemba 9 kutoka Ujerumani alikokamata nafasi ya pili kwenye riadha za ISTAF nyuma ya Mwamerika Noah Lyles mnamo Septemba 4. Lyles alitwaa taji la ISTAF kwa sekunde 9.95 akifuatiwa na Omanyala (10.11) na Muingereza Jeremiah Azu (10.16). Raia wa Cuba Joseph Fahnbulleh na Mwamerika Kyree King pia wako katika orodha ya watakaotimka 100m kwenye mashindano hayo ya kiwango cha dhahabu ya Continental Tour.

Wakenya wengine ambao wamethibitisha kushiriki Borisa Hanzekovic ni mshindi wa nishani ya fedha ya Jumuiya ya Madola 10000m Daniel Simiu na bingwa wa dunia 1500m kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 Reynold Cheruiyot watakaokimbia 3000m. Pia, kuna bingwa wa dunia Under-20 mbio za 3000m kuruka viunzi na maji Faith Cherotich na mshindi wa Afrika 1500m Winny Chebet watakaotimka katika kitengo cha maili moja.

  • Tags

You can share this post!

STAA WA SPOTI: Ni mfalme mpya Diamond League

TAHARIRI: Mvutano wanukia Mwendwa kusema amerudi afisini FKF

T L