• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Mvutano wanukia Mwendwa kusema amerudi afisini FKF

TAHARIRI: Mvutano wanukia Mwendwa kusema amerudi afisini FKF

NA MHARIRI

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Nchini FKF Nick Mwendwa alitangaza jana kwamba amerejea katika uongozi wa shirikisho hilo baada ya kuwa kwenye kibaridi kwa muda mrefu.

Katika barua aliyoandikia Rais wa FIFA Gianni Infantino, Mwendwa anadai kwamba mashtaka ya ufisadi aliyokuwa akipambana nayo yalishaondolewa na hivyo basi amerejea ofisini. Ni madai ambayo yalikanushwa mara moja na Afisi ya Mashtaka ya Umma kupitia kwa naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Joseph Riungu (habari kamili Uk19) aliyesema kesi za Mwendwa bado zinaendelea na kwamba tarehe ya kusikizwa ni Septemba 21 na 26.

Kwa wachanganuzi na wadadisi wa masuala ya umma, huenda hatua ya Mwendwa inatokana na kuhisi kwamba kuna serikali mpya inayoanza kuchukua mamlaka Jumanne wiki ijayo wakati ambapo Rais Mteule William Ruto ataapishwa. Na hii inatokana na madai yake ya mara kwa mara kwamba mashtaka aliyofunguliwa na Waziri wa Michezo Amina Mohamed yalichochewa kisiasa na kwamba hayana msingi wala mashiko.

Lakini kwa upande mwingine, wadau wanatarajia kwamba sheria itachukua mkondo wake na kesi hizo zimalizike kisheria; kama inavyofanyika kwa Wakenya wote wanaojipata wakikabiliana na mkono wa sheria. Isisahaulike kwamba ukaguzi wa matumizi ya fedha katika shirikisho hilo ulionyesha kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa pesa.

Kwa hivyo, Wakenya wanajipata katika njia panda kuhusu utata huu. Je, ni upande upi unaaminika? Ni upande upi ulio na haki? Ni Mwendwa anayehisi ana nafasi ya kuanza upya maisha kufuatia kuchaguliwa kwa serikali mpya?

Kwenye barua yake amesema kwamba atafanya mikakati kuhakikisha kwamba ile marufuku ya Fifa ambayo imekuwa ikiumiza soka nchini inaondolewa. Na kwa kweli hilo ni jambo ambalo wadau wengi wanataka mno lifanyike kwa sababu hata washindi wa Ligi Kuu, wanakosa kipute cha CAF kutokana na marufuku hiyo.

Ni mtazamo wetu kwamba pande zote husika zitulize boli ili kuepuka kuchanganya umma na wadau kwa jumla. Ikiwa kuna kesi zinazomwandama Mwendwa kama inavyodai afisi ya ODPP, basi hana budi kujiwasilisha kortini na kuwajibikia kesi hizo.
Ana uwezo wa kuwasilisha ombi la kutaka mashtaka hayo yaondolewe kisheria endapo atadhihirishia mahakama kwamba hakuna ushahidi dhidi yake, na washtakiwa wengi washawahi kufaulu katika hilo.

Kile hakipaswi kufanyika ni kwa Mwendwa kupuuza mahakama na kuchukua hatua kama ambaye sheria hazimhusu yeye.

You can share this post!

Omanyala kupimana ubabe na Mwamerika Bracy jijini Zagreb

Utaratibu uliofuatwa kabla ya kutangaza kifo cha Malkia...

T L