• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Real Madrid kuwatia mnadani wanasoka sita mwishoni mwa msimu huu ili wajinasie huduma za Mbappe na Haaland

Real Madrid kuwatia mnadani wanasoka sita mwishoni mwa msimu huu ili wajinasie huduma za Mbappe na Haaland

Na MASHIRIKA

REAL Madrid watawatia mnadani wanasoka sita mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21 ili wawezeshwe kuwasajili Kylian Mbappe na Erling Haaland kutoka Paris Saint-Germain (PSG) na Borussia Dortmund mtawalia.

Kati ya masogora sita hao watakaouzwa na kocha Zinedine Zidane ni Eden Hazard na Gareth Bale ambaye kwa sasa anachezea Tottenham Hotspur kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Japo Dortmund wamefichua kwamba hawana mpango wa kuuza Haaland, kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) huenda kikachochewa kukubali kima cha Sh21 bilioni kutoka kwa Real. Mbali na Real, mwanasoka huyo raia wa Norway anahemewa pia na Manchester United, PSG, Bayern Munich, Liverpool na Chelsea.

Real watahitajika pia kuweka mezani takriban Sh20 bilioni ili kujinasia huduma za Mbappe ambaye angali na mkataba wa kuchezea PSG hadi mwisho wa msimu wa 2022.

Ingawa si matamanio ya PSG kumwachilia Mbappe, fowadi huyo raia wa Ufaransa amewahi kusisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake kitaaluma ni kuchezea Real.

Wanasoka wengine ambao Real watalazimika kuuza ili kujinasia huduma za Mbappe na Haaland ni Sergio Ramos, Raphael Varane, Hazard, Roman Isco na Marcelo Vieira.

Mazungumzo kuhusu uwezekano wa Ramos, 34. kurefusha mkataba wake kambini mwa Real kwa miaka mitatu zaidi yamegonga mwamba sasa beki na nahodha huyo atalazimika kuondoka ugani Santiago Bernabeu baada ya kusakatia Real kwa miaka 16.

Varane anahusishwa pakubwa na Olympique Lyon ya Ufaransa huku Isco na Marcelo ambao makali yao yameshuka pakubwa kambini mwa Real wakihusishwa na uwezekano wa kutua Arsenal.

Hazard aliyesajiliwa na Real kutoka Chelsea, amekuwa mwepesi wa kupata majeraha mabaya ya mara kwa mara.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lukaku avunia Ubelgiji alama moja dhidi ya Jamhuri ya Czech

Uholanzi wajinyanyua na kutandika Latvia 2-0 katika mechi...