• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Real Madrid wakomoa Atletico kwenye gozi kali la Madrid

Real Madrid wakomoa Atletico kwenye gozi kali la Madrid

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walishinda mechi ya 10 mfululizo na kufungua mwanya wa alama nane kileleni mwa jedwali baada ya kupepeta Atletico Madrid 2-0 katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili usiku.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 42. Sevilla wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 34, moja zaidi kuliko Real Betis na tano kuliko mabingwa watetezi Atletico wanaofunga mduara wa nne-bora.

Karim Benzema ambaye ni mfungaji bora kwa sasa katika La Liga, aliwaweka Real kifua mbele baada ya kushirikiana na Vinicius Jr katika dakika ya 16. Vinicius ndiye aliyechangia pia bao la pili lililofumwa wavuni na Marco Asensio katika dakika ya 57.

Real wamepoteza mara mbili pekee kutokana na mechi 23 zilizopita. Miamba hao hawajapoteza mchuano wowote tangu Oktoba 3 na tangu kocha Ancelotti aaminiwe kuwa mrithi wa mkufunzi Zinedine Zidane.

Atletico walipoteza nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha pili kupitia Antoine Griezmann aliyemtatiza pakubwa kipa Thibaut Courtois.

Bao la Benzema lilikuwa lake la 13 katika La Liga msimu huu na 36 akivalia jezi za Real katika kampeni za mashindano yote mengine mwaka huu wa 2021. Hiyo ndiyo rekodi nzuri zaidi anayojivunia katika historia yake ya usogora. Nyota huyo raia wa Ufaransa aliondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza na nafasi yake kutwaliwa na Luka Jovic.

Kwa upande wao, Barcelona walishuka hadi nafasi ya nane jedwalini kwa alama 18 nyuma ya Real baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Osasuna.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mbappe aongoza PSG kuzamisha Monaco ligini

16-BORA UEFA: Man-United kukwaruzana na Atletico nayo Real...

T L