• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Safari Rally balaa!

Safari Rally balaa!

Na GEOFFREY ANENE

MADEREVA walihangaishwa katika siku ya pili ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally zilizoendelea kudumisha hadhi yake kama mashindano magumu kabisa duniani ya magari.

Mbelgiji Thierry Neuville (Hyundai i20) alimaliza siku akiwa kileleni, ingawa hakuna dereva hata mmoja wa magwiji wote wanaoshikilia nafasi 10 za kwanza duniani wanaoshiriki Safari Rally, waliepuka taabu.

Mshindi wa duru ya Ureno, Elfyn Evans kutoka Uingereza (Toyota Yaris), Mhispania Dani Sordo (Hyundai i20), Mswidi Oliver Solberg (Hyundai i20) na Mwitaliano Lorenzo Bertelli (Ford Fiesta) walisalimu amri ya barabara hizo za vumbi na mawe katika maeneo tofauti ya mashindano katika eneobunge la Naivasha baada ya kukumbwa na matatizo.

Bingwa mara saba duniani Sebastien Ogier kutoka Ufaransa alilazimika kujikokota hadi kituo cha kurekebisha magari baada ya gari lake la Toyota Yaris kuharibika “suspension” kati ya mkondo wa tatu (Kedong) na ule wa nne (Oserian).

Alilirekebisha na kuendelea na mashindano.Neuville alipata panchari mbili mara moja katika mkondo wa nne.Hata hivyo, tukio baya hiyo jana lilihusisha Mkenya Tejveer Rai.

Gari lake la Volkswagen Polo liligonga mwinuko na kuruka kabla ya kugeuka magurudumu juu katika mkondo wa tatu. Baada ya kuandikisha kasi bora katika mkondo mfupi wa kilomita 4.84 katika eneo la Kasarani jijini Nairobi mnamo Alhamisi, Ogier ndiye alikuwa wa kwanza kutoka jukwaani siku ya pili.

Alifuatiwa na Evans, Neuville, raia wa Estonia Ott Tanak ambaye ni bingwa wa dunia 2019 na Mjapani Takamoto Katsuta katika nafasi tano za kwanza.Neuville anayeendesha gari aina ya Hyundai alishinda mkondo wa pili Chui Lodge (kilomita 13.34) na tatu Kedong (32.68) kwa dakika 42 na sekunde 48.9.

Aliongoza Kalle Rovanpera wa Toyota kwa sekunde 5.1.Raia wa Finland, Rovanpera alipata panchari katika eneo la Kedong.

Alishinda mkondo wa nne katika eneo la Oserian (18.87km). Hata hivyo, hakuwa na lake katika mkondo wa kufunga siku alipokwama kwenye changarawe.Evans alijiuzulu mashindano ya siku ya kwanza gari lake lilipoharibika katika mkondo wa tatu.

“Tumelazimika kumaliza mashindano mapema leo kwa sababu tumegonga jiwe na gari letu kuharibika “suspension”. Ni aibu kubwa kuwa hatutapata kufurahia mikondo mingine ya leo (jana),” alisema mwelekezi wake Scott Martin.

Sordo pia alilazimika kusimamisha gari lake katika mkondo huo alipopotea barabara akiendesha gari lake la Hyundai.

“Leo (jana), tumejifundisha kuwa sio simba hung’ata, bali pia Safari Rally,” alisema. Baada ya siku ya pili, Neuville anaongoza mbio hizo za kilomita 320.19 kwa saa moja, dakika 23 na sekunde 19.1. Katsuta (1:23:37.9), Tanak (1:24:14.9) na Ogier (1:25:08.5) walifuatana katika nafasi nne za kwanza.

You can share this post!

Waziri Mkuu wa Algeria ajiuzulu

DOUGLAS MUTUA: Haji asihofie ugumu wakazi, aendelee...