• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Safari ya Ndula FC katika bahari ya kandanda

Safari ya Ndula FC katika bahari ya kandanda

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya Ndula FC ya Thika Mashariki, imekuwa katika ulingo wa michezo kwa miaka sita mfululizo kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana.

Kocha wake Jackton Omondi anasema timu hiyo iko chini ya usimamizi wa kampuni ya kutengeneza juisi ya matunda ya mananasi ya Delmonte Ltd iliyoko mjini Thika.

Anasema ya kwamba mara yake ya kwanza wakati anabuni klabu hiyo alikuwa na changamoto tele kwa sababu vijana wa kijiji cha Ngoliba, hawakuwa na ustadi wowote wa kusakata kabumbu.

Kwa hivyo mwaka wa 2016, alilazimika kusafiri hadi maeneo ya Magharibi na Nyanza ili kusaka vijana waliokuwa na uwezo wa kugaragaza boli uwanjani.

“Kwa hivyo kampuni iliniruhusu kuunda kikosi kamili cha soka na nilifanya juhudi na kupata vijana wapatao 18,” kocha huyo anasema.

Alipata vijana kadha na waliweza kuunda kikosi cha soka ambapo wote walikubali kusajiliwa na kuunda timu ya Ndula FC.

Anaeleza kuwa aliwaongoza kucheza mechi za kirafiki na za mataji huku vijana hao wakiendelea kuonyesha ujabali wao.

“Ama kwa hakika ninajivunia kuwa kocha wa timu hiyo kwa sababu kwa muda mrefu kampuni ya Delmonte imekuwa mstari wa mbele kuwafadhili vijana hao kwa kuwapa vifaa muhimu na hata usafiri wakienda kushiriki mechi za maeneo ya mbali,” anafafanua kocha huyo.

Anaipongeza kampuni hiyo kwa kufanya juhudi kuajiri kazi vijana wapatao 22 miongoni mwa 30 ambao wanaunda kikosi chote cha Ndula kwa sasa.

Anasema mwaka wa 2020 klabu hiyo ilishiriki katika Ligi ya Zoni D kanda ya Kati ambapo waliweza kuzoa pointi 36.

Hata hivyo, anasema kikosi chake kinazingatia mazoezi ya kila mara huku vijana wakidumisha nidhamu ya hali ya juu.

“Mara nyingi nimekuwa nikiwarai vijana hao wawe wachezaji wenye nidhamu ili waweze kupiga hatua zaidi kimchezo. Kila mchezaji ana nafasi yake ya kufanya vyema,” alieleza kocha huyo.

Alipongeza mashabiki wao ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwapa motisha kufanya vyema uwanjani.

Anasema tayari timu hiyo imelipa fedha za kushiriki – Sh45,000 – lakini kile wanachokosa kwa sasa ni vifaa kamili vya michezo kama jezi, viatu na mipira.

“Hata ingawa kampuni inajitolea na misaada ya usafiri na na fedha za kushiriki ligi hiyo, ukweli wa mambo ni kwamba hata mimi kama kocha na wahisani wachache tunajitolea mhanga kununua vifaa vichache vya michezo kama mipira na kulipa marefarii,” anasema.

Hata hivyo anawasifu maafisa kadha ambao wanasaidiwa kuendesha kikosi hicho.

Kuna meneja ambaye ni Elly Tormoi, msaidizi wa kocha ni Philip Ayunda naye mkufunzi wa makipa ni Shadrack Okello.

  • Tags

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Raila asipotoshwe; anaweza kushinda bila...

‘Jungle’ ajitenga na harakati za chama cha UDA

T L