• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Saudi Arabia yaduwaza dunia baada ya kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Argentina 2-1 katika Kundi C

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Saudi Arabia yaduwaza dunia baada ya kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Argentina 2-1 katika Kundi C

Na MASHIRIKA

LIMBUKENI Saudi Arabia walitoka nyuma na kupepeta Argentina 2-1 katika miongoni mwa matokeo ya kuduwaza zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.

Kikosi hicho cha Mashariki ya Kati kilishuka dimbani kikiwekewa matumaini finyu ya kutatiza Argentina – mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia (1978, 1986) walioshuhudia mabao yao matatu yakikosa kuhesabiwa kwa madai kuwa wafungaji walicheka na nyavu wakiwa wameotea.

Argentina walianza mechi kwa matao ya juu na wakawekwa kifua mbele na supastaa Lionel Messi kunako dakika ya 10. Hata hivyo, Saudi Arabia almaarufu

Green Falcons walisawazisha kupitia kwa Saleh Al Shehri katika dakika ya 48 kabla ya Salem Al Dawsari kupachika wavuni bao la ushindi dakika tano baadaye.

Ushindi wa Saudi Arabia ulikuwa wao wa nne katika historia ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Kwa kushinda Argentina, walipaa hadi kileleni mwa Kundi C kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Poland na Mexico walioambulia sare tasa katika pambano jingine la kundi hilo.

Chini ya kocha Lionel Scaloni, Argentina walionyanyua taji la Copa America 2021, walijibwaga ulingoni wakipigiwa upatu wa kuchangamkia Saudi Arabia bila huruma na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 36 mfululizo.

Sasa wana kibarua kigumu cha kuzamisha Mexico mnamo Novemba 26 na kuweka hai matumaini ya kutawazwa mabingwa wa dunia kwa mara ya tatu katika historia na kuaga Messi kwa taadhima ya kipekee.

Huku Argentina wakijiandaa kuvaana na Mexico, Saudi Arabia watapepetana na Poland katika pambano lao la pili la Kundi C.

Argentina ni miongoni mwa vikosi vya haiba kubwa zaidi nchini Qatar vinavyopigiwa upatu wa kunyanyua Kombe la Dunia mwaka huu kutokana na wingi wa wachezaji wazoefu kikosini mwao.

Mnamo 2018, walidenguliwa na Ufaransa kwa kichapo cha 4-3 katika hatua ya 16-bora. Walifungua kampeni zao za Kundi D kwa sare ya 1-1 dhidi ya Iceland kabla ya Croatia kuwapepeta 3-0. Walikamilisha mechi za makundi kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Nigeria.

Lakini chini ya Scaloni, Argentina wamekuwa wakijivunia ufufuo mkubwa wa makali yao huku wakifunga mabao 16 na kutoruhusu wapinzani kuwafunga bao lolote kutokana na mechi tano walizozitandaza kabla ya kufunga safari ya kuelekea Qatar.

Saudi Arabia ya kocha Herve Renard ndicho kikosi cha kwanza kisichotokea bara Ulaya kuwahi kupepeta Argentina katika mechi ya Kombe la Dunia baada ya Cameroon mnamo 1990.

Licha ya kichapo hicho cha miaka 32 iliyopita, Argentina bado walitinga fainali ya kipute hicho kilichofanyika Italia na kutamalakiwa na Ujerumani.

Mbali na kichapo cha 2-1 ambacho Argentina walipokezwa na Saudi Arabia, matokeo mengine ya kushangaza zaidi katika historia ya Kombe la Dunia ni ushindi wa Amerika dhidi ya Uingereza mnamo 1950 na kichapo ambacho Algeria walipokeza Ujerumani mnamo 1982.

Kabla ya Saudi Arabia, vikosi vitatu vya mwisho kuwahi kuangusha Argentina katika Kombe la Dunia viliishia kunyanyua taji la kipute hicho au kutinga fainali – Ujerumani na Ufaransa walitawazwa wafalme mnamo 2014 na 2018 mtawalia huku Croatia wakiingia fainali.

Mara ya mwisho kwa Saudi Arabia kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia ni 1994.

MATOKEO YA KUDUWAZA ZAIDI KATIKA HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA:

MATOKEO MWAKA
Saudi Arabia 2-1 Argentina 2022
Uswisi 1-0 Uhispania 2010
Ghana 2-0 Jamhuri ya Czech 2006
Algeria 2-1 Ujerumani 1982
Amerika 1-0 Uingereza 1950

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Tunisia na Denmark waumiza bure nyasi za uwanja wa...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Poland na Mexico watoshana nguvu...

T L