• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Tunisia na Denmark waumiza bure nyasi za uwanja wa Education City katika mchuano wa Kundi D

Tunisia na Denmark waumiza bure nyasi za uwanja wa Education City katika mchuano wa Kundi D

Na MASHIRIKA

DENMARK na Tunisia walitoshana nguvu katika mechi ya Kundi D iliyowakutanisha uwanjani Education City, Al Rayyan.

Licha ya kuwajibisha idadi kubwa ya wanasoka wazoefu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Denmark walitatizwa na Tunisia waliotawazwa wafalme wa Afrika mnamo 2004.

Kiungo Christian Eriksen, aliyepata tatizo la moyo akichezea Denmark dhidi ya Finland katika mchuano wa kwanza wa fainali za Euro 2020 mnamo Juni 2021, alidhibitiwa vilivyo na mabeki wa Tunisia katika vipindi vyote viwili.

Jaribio lake la pekee langoni mwa Tunisia ni kombora alilovurumisha katika kipindi cha pili ila likadhibitiwa vilivyo na kipa Aymen Dahmen.

Vikosi vyote viwili vilishuhudia mabao yao yakifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR baada ya kubaini kuwa wafungaji walicheka na nyavu wakiwa wameotea.

Andreas Cornelius alipoteza nafasi nyingi za wazi za kufungia Denmark waliolalamikia kunyimwa penalti na refa Cesar Ramos sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Kwenya fainali za Euro 2020, Denmark walitamba pakubwa hadi wakaingia hatua ya nusu-fainali. Walishuka dimbani dhidi ya Tunisia wakipigiwa upatu wa kulaza Tunisia ikizingatiwa kwamba walikuwa wameshinda mechi tisa kati ya 10 za kujikatia tiketi ya kuelekea Qatar mwaka huu.

Chini ya kocha Kasper Hjulmund, Denmark sasa wanajiandaa kuvaana na Ufaransa katika pambano lao lijalo mnamo Novemba 26 huku Tunisia wakimenyana na Australia waliofungua kampeni zao kwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa mabingwa watetezi, Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali ifanikishe mpango wa kupunguza...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Saudi Arabia yaduwaza dunia baada...

T L