• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Shujaa yarejea nyumbani na majeraha Kabras ikikwamilia juu ya ligi ya Kenya Cup

Shujaa yarejea nyumbani na majeraha Kabras ikikwamilia juu ya ligi ya Kenya Cup

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande maarufu kama Kenya Shujaa imerejea nyumbani Jumapili kutoka nchini Milki za Kiarabu jana alasiri ikiuguza majeraha mawili.

Shujaa ilizoa alama jumla ya alama 22 kutoka duru mbili za kwanza za Raga za Dunia jijini Dubai zilizoandaliwa Novemba 26-27 na Desemba 3-4. Kocha Innocent “Namcos” Simiyu alieleza Taifa Leo kuwa mchezaji Daniel Taabu kutoka klabu ya Mwamba na Nelson Oyoo (Top Fry Nakuru) walijeruhiwa mguu na kifundo katika duru ya pili ya Dubai Sevens mtawalia.

Kuhusu matokeo ya Shujaa, Namcos alisema, “Kwa jumla, matokeo yalikuwa sawa. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya, lakini tunashukuru kuwa tumekuwa na mwanzo mzuri kwa msimu baada ya muda mrefu.” Kenya, ambayo itarejelea mazoezi Jumatano ijayo, inakamata nafasi ya nane kwa alama 22 ikiwa nyuma ya Afrika Kusini (44), Argentina (34), Australia (32), Amerika (30), Great Britain (25), Fiji (23) na Ufaransa (23) mtawalia.

Aidha, Kabras Sugar inasalia juu ya jedwali la Ligi Kuu nchini (Kenya Cup) kwa alama 10 ikifuatiwa Strathmore Leos na Menengai Oilers kwa tofauti ya ubora wa ukubwa wa ushindi nazo Kenya Harlequin na Masinde Muliro (MMUST) zimezoa pointi tisa na nane mtawalia.

Mabingwa watetezi KCB wako katika nafasi ya sita kwa alama nne baada ya mchuano wao wa pili dhidi ya Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kuahirishwa Jumamosi.

You can share this post!

Wafuasi wa Hasla wakosoa Rais ‘kudai amestawisha kilimo’

TAHARIRI: Chanjo kwa wingi itasaidia kukabiliana na corona...

T L