• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Southampton wakomoa Brentford na kupaa kwenye jedwali la EPL

Southampton wakomoa Brentford na kupaa kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

SOUTHAMPTON walichupa hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 24 baada ya kupepeta limbukeni Brentford 4-1 katika uwanja wa St Mary’s mnamo Jumanne usiku.

Jan Bednarek aliwaweka wenyeji kifua mbele baada ya kushirikiana na James Ward-Prowse katika mchuano huo uliohudhuriwa pia na mmiliki mpya wa Southampton, Dragan Solak.

Brentford walisawazisha kupitia Vitaly Janelt aliyekamilisba krosi ya Bryan Mbeumo kunako dakika ya 23. Hata hivyo, Southampton walirejea uongozini kupitia Ibrahima Diallo aliyemzidi ujanja kipa Alvaro Fernandez katika dakika ya 37.

Bao la tatu la Southampton lilifumwa wavuni kupitia Armando Broja aliyeshirikina na Oriel Romeu katika dakika ya 49 kabla ya Che Adams kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao kunako dakika ya 70.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Southampton kufunga mabao manne katika mchuano mmoja wa EPL msimu huu wa 2021-22.

Aidha, ilikuwa mechi ya kwanza kwa Southampton kusakata tangu kampuni ya Sport Republic inayomilikiwa na mwanahabari bwanyenye raia wa Serbia, Solak, kutwaa umiliki wa hisa 80 za mfanyabiashara wa China, Gao Jisheng kambini mwa kikosi hicho mwanzoni mwa Januari 2022.

Ushindi uliwawezesha Southampton kuruka Brentford ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya 13 kwa alama 23 sawa na Crystal Palace ya kocha Patrick Vieira.

Brentford walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kutamba baada ya fowadi wao tegemeo Mbeumo kufunga mabao matatu katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Port Vale katika raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 8, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wandani wa Kalonzo wapuuzilia mbali ‘njama’ ya...

Staa wa Bandari FC Shaaban Kenga kurudi uwanjani

T L