• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Spurs watoka nyuma na kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Southampton katika EPL

Spurs watoka nyuma na kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Southampton katika EPL

Na MASHIRIKA

PENALTI iliyofungwa na mshambuliaji Son Heung-min katika dakika za mwisho iliwasaidia Tottenham Hotspur kusajili ushindi muhimu wa 2-1 dhidi ya Southampton katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatano usiku jijini London.

Ni matokeo ambayo yalimshuhudia kocha mshikilizi Ryan Mason, 29, akianza vyema kibarua cha kudhibiti mikoba ya Spurs baada ya kuaminiwa kujaza pengo la Jose Mourinho hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21. Mourinho almaarufu ‘The Special One’ alifutwa kazi na Spurs mnamo Aprili 19, 2021 baada ya miezi 17.

Mason ambaye ni kiungo wa zamani wa Spurs, kwa sasa ndiye mkufunzi mchanga zaidi katika soka ya EPL. Alistaafu kwenye ulingo wa usogora mnamo 2018 baada ya kupata jeraha baya la kichwa.

Katika mtihani wake wa kwanza, alishuhudia fowadi Gareth Bale akiwafungulia Spurs ukurasa wa mabao katika dakika ya 60 baada ya kusawazisha goli ambalo Danny Ings alifungia Southampton kunako dakika ya 30.

Son alifungia waajiri wake goli la pili katika dakika ya 90 baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba beki Moussa Djenepo alimchezea vibaya kiungo Harry Winks ndani ya kijisanduku chao. Bao la Ings lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na James Ward-Prowse.

Spurs waliokosa maarifa ya mfumaji na nahodha Harry Kane katika mchuano huo, walisalia kumtegemea pakubwa Son aliyeshirikiana na Bale pamoja na Lucas Moura katika safu ya uvamizi.

Alama tatu zilizovunwa na Spurs dhidi ya Southampton almaarufu ‘The Saints’ ziliwakweza hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali. Kikosi hicho kwa sasa kinajiandaa kuvaana na Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 25, 2021.

Spurs wamejizolea jumla ya alama ya 53 kutokana na mechi 33 zilizopita ligini. Alama zao zinawiana na zile ambazo Liverpool wametia kapuni baada ya kusakata jumla ya mechi 32 kufikia sasa msimu huu.

Kwa upande wao, Southampton wanaonolewa na kocha Ralph Hassenhutl wanakamata nafasi ya 14 jedwalini kwa pointi 36, tisa nje ya mduara unaojumuisha vikosi vya Fulham na West Bromwich Albion vilivyo katika hatari ya kuteremshwa ngazi kwenye EPL msimu huu baada ya Sheffield United.

Wakiwa tayari wamebanduliwa kwenye soka ya Europa League na kujivunia alama tano pekee kutokana na 15 zilizopita, Spurs walishuka dimbani dhidi ya Southampton wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua na kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Baada ya kuonana na Man-City kwenye fainali ya Carabao Cup, Spurs watarejea kunogesha kivumbi cha EPL dhidi ya Sheffield United mnamo Mei 2, siku tatu baada ya Southampton kumenyana na Leicester City ugani St Mary’s, Uingereza.

MATOKEO YA EPL (Aprili 21, 2021):

Tottenham 2-1 Southampton

Aston Villa 1-2 Man-City

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid wachabanga Cadiz na kupaa hadi kileleni mwa...

Inter Milan sasa pua na mdomo kutwaa taji la Serie A kwa...