• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Thika Queens warambwa na Vihiga Queens, Gaspo nao watandika Kisumu All Starlets

Thika Queens warambwa na Vihiga Queens, Gaspo nao watandika Kisumu All Starlets

NA AREGE RUTH

MASAIBU ya mabingwa watetezi Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) Thika Queens yameendelea kushuhudiwa ligini baada ya kichapo cha 1-0 kutoka kwa Vihiga Queens ugani Moi jijini Kisumu mnamo Jumamosi.

Sajili mpya Bertha Omitta ametonesha kidonda cha Thika kwa kufunga bao dakika ya 41. Ushindi huo, unaendelea kuiweka Vihiga nafasi ya pili na alama 43 sawa na vinara wa ligi Gaspo Women.

Thika chini ya kocha Fredrick Majani, sasa wamepokea kichapo chao cha saba msimu huu na wameganda nafasi ya sita na alama 27.

Ugani GEMS Cambridge, Gaspo Women wamehakikisha Kisumu All Starlets wanarejea ‘Kisumu Dala’ mikono mitupu kwa kuwanyorosha 3-0.

Mshambulizi matata Lydia Akoth alicheka na wavu mapema dakika ya 10 na kuwafanya Gaspo kuongoza katika kipindi cha kwanza.

Mambo yalizidi unga kipindi cha pili. Kocha wa makipa wa Gaspo James Ombeng’, alifanya mabadiliko katika safu ya mashambulizi.

Lyvne Achola aliingia kuchukua nafasi ya Ann Nabwire dakika ya 55.

Kutokana na uzoefu wake wakuchenga, alifunga bao la pili dakika ya 20 kutumia mguu wa kushoto baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Kisumu Maureen Awiti, Vivian Nancy na Teresa Makokha.

Naye Akoth alifunga kazi ya siku kwa kufunga bao lingine dakika za lala salama kipindi cha pili.

Mabao ya washambulizi Mercy Airo na Fasila Adhiambo dakika ya 20 na 75 mtawalia, yalitosha kuwapa wanajeshi wa Ulinzi Starlets alamu tatu muhimu dhidi ya Wadadia Women ugani Mumias Sports Complex.

Katika mechi tano za awali, Ulinzi wamepata ushindi mara nne na kuandikisha sare moja. Wamefunga tatu bora kwenye msimamo wa ligi na alama 38 kutokana na mechi 18.

Wadadia ambao wako nafasi ya nne na alama 32, wameshinda mechi 10 sare mbili na kupoteza mechi sita.

  • Tags

You can share this post!

Lesiit ateuliwa kuongoza jopo la Shakahola

Rais wa tenisi ya mezani duniani apongeza Kenya kwa kuandaa...

T L