• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Timu kubwa Kenya zaumia kutokana na ukosefu wa viwanja

Timu kubwa Kenya zaumia kutokana na ukosefu wa viwanja

Na JOHN ASHIHUNDU

UKOSEFU wa viwanja vya kisasa katika Kaunti ya Nairobi unaendelea kuumiza timu za Ligi Kuu huku wachezaji wakiendelea kujeruhiwa kila wakati.

Tatizo hili linachangia matokoe duni kwa timu za AFC Leopards, Gor Mahia, Kariobangi Sharks, Kenya Commercial Bank (KCB) pamoja na Nairobi City Stars.

Kati ya timu zote 18 za ligi hiyo kuu, ni Tusker pekee walio na uwanja wao mtaani Ruaraka kwa sasa.

Licha ya kujivunia ufuasi mkubwa wa mashabiki, AFC Leopards na Gor Mahia ni miongoni mwa timu ambazo licha ya kuanzishwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, zinaendelea kukodi viwanja vya kuchezea mechi zao za nyumbani.

Kwa sasa, timu hizo ni miongoni mwa zinazotumia uwanja wa nje wa MISC, Kasarani huku ardhi yao waliopewa na Marehemu Mzee Daniel Arap Moi zikiendelea kumilikiwa na watu wasio na makao tangu mapema miaka ya tisini.

Timu hizi ambazo zilitumia Nyayo kwa mechi zao za nyumbani hazijakubaliwa kurejea uwanjani humo tangu ufanyiwe marekebisha makubwa na kukamilika miezi sita iliyopita.

Asilimia 50 ya timu za ligi kuu zinatoka Nairobi, lakini hazina viwanja vya kuchezea mechi zao.

Viongozi wa timu hizo, akiwemo mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda ni miongoni mwa wanaolalamika kuhusu hali ya uwanja wa MISC, Kasarani ambao wanadai umechakaa.

Jinsi uwanja huu unavyozidi kuchakaa, kuna uwezekano wa timu kadhaa kuanza kutafuta viwanja vilivyo nje ya jiji hili.

Miongoni mwa viwanja hivyo ni Narok Stadium na Mwanyumba katika eneo la Taita Taveta, lakini itabidi zitumie pesa nyingi kusafirisha wachezaji kila mara.

Ukosefu huu wa viwanja umechangia katika mechi kadhaa kusukumwa mbele kuupa uwanja wa MISC Kasarani muda wa kurudia katika hali nzuri.

Shikanda anadai kwa siku moja timu yake itahitaji Sh250,000 kagharamia mechi yao kuchezewa Narok, wakati ni Sh85,000 pekee kuchezea Nairobi.

Majuzi, klabu ya Wazito FC ililazimika kuchezea mechi yao ugani Bukhungu mjini Kakamega dhidi ya Zoo Kericho ilhali makao yake ni Nairobi.

Mkurugenzi wa Michezo, Stephen Ochiel amethibitisha kwamba ni gharama kubwa kwa timu za Nairobi kuchezea mechi zao nje ya Nairobi.

Serikali imetoa ilani kwamba uwanja wa Nyayo huwezi kutumika kwa mechi za ligi, na hadi sasa timu zinasubiri kwa hamu kuambiwa wakati zitarejea uwanjani humo kufurahia uhondo.

Mkurugenzi wa Sports Kenya, Pius Meto alisema timu zimepigwa marufuku kuchezea uwanjani humo kufuatia uharibifu uliotokana na mashabiki wenye vurugu.

Alisema timu zimetuma maombi ya kutaka kuchezea mechi zao uwanja humo, lakini kwa sasa haitawezekana.

Meto hata hivyo alisisitiza kwamba kufikia katikati mwa mwaka huu, Kenya itakuwa na viwanja vya kutosha huku akitarajia shida za viwanja kumalizika.

Mbali na ukosefu huu wa viwanja vya kuchezewa mechi kubwa, kadhalika Serikali imeshindwa kuboresha viwanja vya michezo kutokana na kunyakuliwa kwa ardhi ya umma na watu binafsi kote nchini.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo hakuna viwanja vya umma ambavyo vinaweza kutumika kwa shughuli za michezo.

Alisema viwanja vichache vya serikali za kaunti vinahitaji fedha nyingi kukarabati, wakati huu serikali haina pesa.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa shawarma ya minofu ya kuku

Matiang’i asisitiza haja ya mahakama, DCI na DPP...