• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Timu za Afrika zaendelea kulemewa Qatar

Timu za Afrika zaendelea kulemewa Qatar

Na JOHN ASHIHUNDU

MATUMAINI ya timu za Afrika kupiga hatua kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022 yalizidi kudidimia baada ya kikosi cha Cameroon kuchapwa 1-0 na Uswisi katika mechi iliyochezewa Janoub Stadium leo, Alhamisi.

Mbali na Cameroon, mataifa mengine ya Afrika yanatoshiriki kwenye fainali hizo ni Morocco, Senegal, Tunisia na Ghana, lakini tukienda mitamboni, hakuna timu ya Afrika iliyoanza kwa ushindi.

Senegal waliowekewa matumaini ya kufanya makubwa kwa kuwa ndoo mabingwa wa Afrika, mbali na kuorodheshwa katika nafasi ya kwanza kwa timu za Afrika kwenye viwango vya kimataifa vya Fifa, ilianza kwa kuchapwa 2-0 na Uholanzi.

Baadaye, Morocco na Tunisia zikatoka sare dhidi ya Croatia na Denmark mtawaliwa, na wakati tukiandika habari hizi, Ghana ilikuwa ikijiandaa kuvaana na Ureno ya Cristiano Ronaldo kuanzia saa moja usiku.

Mashabiki kadhaa wameanza kuwa na wasiwasi kufuatia matokeo hayo duni, ambayo inasemekana huenda yanachangiwa na timu za Afrika kuwa na wachezaji wachache wa viwango vya juu, ikilinganishwa na wapinzani wao kutoka mataifa ya Ulaya na Amerika Kusini.

Timu za Afrika zimekosa wachezaji walio na uzoefu kama ilivyokuwa wakati wa akina Roger Milla aliyeongoza Cameroon kutinga hatua ya robo-fainali.

Imefahamika kwamba kushindwa kwa timu za Afrika mapema kunatokana na kutegemea wachezaji wachache kikosini.

Kwa mfano, wakati Senegal inamtegemea Sadio Mane anayeuguza jeraha, Morocco itawategemea Acharaf Hakimi, Hakim Ziyech na Noussair Mazraoui.

Timu nyingine inayowakilisha Afrika – Tunisia inategemea Hannibal Mejbri, Youssef Msakni, Issam Jebali na Seifeddine Jaziri ambao katika mechi yao ya ufunguzi, hawakuonyesha makali yao kama ilivyotarajiwa.

Ghana inayotegemea akina Thomas Partey, Mohammed Kudus na Alexander Djiku imebadilika kabisa, ambapo nyota maarufu kama Asamoah Gyan, na Andre Ayew wenye ujuzi wa kutosha hawapo.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ubelgiji watolewa jasho na Canada...

BI TAIFA, Novemba 24, 2022

T L