• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:26 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ubelgiji watolewa jasho na Canada kabla ya kuvuna ushindi wa 1-0 katika Kundi F

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ubelgiji watolewa jasho na Canada kabla ya kuvuna ushindi wa 1-0 katika Kundi F

Na MASHIRIKA

UBELGIJI walitolewa jasho na Canada kabla ya kusajili ushindi wa 1-0 katika mchuano wa Kundi F kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo Novemba 23 ugani Ahmad Bin Ali.

Canada walitamalaki mchezo na kulemea Ubelgiji katika takriban kila idara ila wakapoteza nafasi nyingi za wazi. Beki Alphonso Davies alipoteza penalti iliyopanguliwa na kipa Thibaut Courtois katika kipindi cha kwanza.

Courtois pia aliwajibishwa vilivyo na Alistair Johnston. Hata hivyo, Canada walitepetea mwishoni mwa kipindi cha kwanza na wakafungwa bao na Michy Batshuayi aliyeshirikiana vilivyo na Toby Alderweireld kumwacha hoi kipa Milan Borjan.

Jonathan David nusura asawazishie Canada katika kipindi cha pili ila Courtois akadhibiti vilivyo kombora lake kabla ya kupangua pia fataki aliyoelekezewa na Cyle Larin.

Mwishoni mwa mechi hiyo, kocha Roberto Martinez alitaka masogora wake wanaoorodheshwa wa pili kimataifa kujituma zaidi katika michuano ijayo ya Kundi F dhidi ya Croatia na Morocco waliofungua kampeni za kundi hilo kwa sare tasa uwanjani Al Bayt.

“Canada walicheza vizuri na kwa kweli walistahili kushinda mechi hii. Japo tumeshinda, tuna ulazima wa kuimarisha zaidi mchezo wetu na kusonga mbele hatua kwa hatua,” akasema Martinez.

Ubelgiji wanajivunia idadi kubwa ya wanasoka wa haiba wakiwemo Kevin de Bruyne, Courtois, Yannick Carrasco na Eden Hazard. Mbali na Romelu Lukaku anayetarajiwa kucheza mechi ijayo dhidi ya Morocco ugani Al-Thumama, kikosi chao pia kina mabeki wazoefu Toby Alderweireld, 33, na Jan Vertonghen, 35.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KINYUA KING’ORI: Serikali itathmini upya mpango wake...

Timu za Afrika zaendelea kulemewa Qatar

T L