• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Tottenham walaza West Ham United na kuingia ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Tottenham walaza West Ham United na kuingia ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur waliweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora baada ya kukomoa West Ham United 2-0 mnamo Jumapili.

Matokeo hayo yaliendeleza masaibu ya kocha David Moyes aliyeshuhudia kikosi chake kikiteremka hadi ndani ya mduara wa timu tatu za mwisho zinazokodolea macho hatari ya kushushwa daraja msimu huu wa 2022-23.

Spurs waliwekwa kifua mbele na Emerson Royal aliyeshirikiana na Ben Davies katika dakika ya 56 kabla ya Son Heung-min kukamilisha krosi safi ya Harry Kane na kupachika wavuni goli la pili kunako dakika ya 72.

West Ham walipoteza fursa nzuri ya kurejea mchezoni kupitia kwa Jarrod Bowen aliyeshindwa kumwacha hoi kipa Fraser Forster licha ya kumzidi ujanja beki Cristian Romero.

Heung-min alicheka na nyavu za wageni wao dakika nne baada ya kuletwa uwanjani katika kipindi cha pili na kumzidi maarifa kipa Lukasz Fabianski.

West Ham wangewaruka Bournemouth na Everton iwapo wangeambulia sare. Hata hivyo, walisalia katika nafasi ya 18 jedwalini kwa alama 20 kutokana na mechi 23. Kichapo kutoka kwa Spurs kilikuwa cha kwanza kwa West Ham kupokezwa baada ya mechi tano za mashindano yote.

Kwa upande wao, Spurs waliwaruka Newcastle United na kupaa hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 42. Ni pengo la pointi 10 ndilo linawatenganisha na mabingwa watetezi Manchester City wanaoshikilia nafasi ya pili.

Tofauti na West Ham waliolazimishia Chelsea sare ya 1-1 katika mchuano wao uliopita ligini, Spurs walipondwa na Leicester 4-1 katika EPL uwanjani King Power siku tatu kabla ya AC Milan ya Italia kuwalaza 1-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya UEFA ugani San Siro.

Wakicheza na West Ham, Spurs walikuwa bila mkufunzi Antonio Conte ambaye ameshauriwa kupumzika hadi atakapopona baada ya kufanyiwa upasuaji tumboni. Kutokuwepo kwa kocha huyo raia wa Italia kulimpisha tena msaidizi wake Cristian Stellini aliyewahi kuongoza Spurs kupiga Man-City 1-0 ligini mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari na kupepeta Olympique Marseille ya Ufaransa 2-1 katika makundi ya UEFA mnamo Novemba 2022.

Spurs walioshinda West Ham 2-1 nyumbani kisha 3-1 ugenini katika EPL msimu jana, waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya masogora hao wa David Moyes katika mkondo wa kwanza wa ligi msimu huu.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Man-United 3-0 Leicester

Tottenham 2-0 West Ham

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Akina mama na vijana ndio waathiriwa wakuu wa demokrasia ya...

Mahakama yakataa kuagiza kesi dhidi ya Obado ianze upya

T L