• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
Tottenham wapitwa na Arsenal baada ya kukabwa koo na Brentford ligini

Tottenham wapitwa na Arsenal baada ya kukabwa koo na Brentford ligini

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Tottenham Hotspur kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya orodha ya nne-bora msimu huu yalififishwa Jumamosi na Brentford waliowalazimishia sare tasa.

Kiungo wa Brentford, Christian Eriksen, aliridhisha zaidi katika mechi hiyo iliyomkutanisha na waajiri wake wa zamani.

Eriksen ambaye ni raia wa Denmark, alikuwa akivaana na Spurs kwa mara ya kwanza tangu aagane na kikosi hicho na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Inter Milan mnamo Januari 2020. Alipokelewa vyema na wanasoka wa Spurs pamoja na mashabiki kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa gozi hilo jijini London kupulizwa.

Nusura mpira wa ikabu alioupiga mwishoni mwa kipindi cha pili ujazwe kimiani na Ivan Toney aliyeshuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Spurs.

Spurs walikosa kuelekeza kombora lolote langoni mwa Brentford katika mechi ya pili mfululizo huku makali ya wavamizi wao, akiwemo nahodha Harry Kane, yakizimwa kirahisi na wenyeji waliotegemea pakubwa huduma za kipa David Raya.

Sare hiyo ilishuhudia Spurs wakiteremka hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 58, mbili nyuma ya Arsenal wanaofunga mduara wa nne-bora. Arsenal waliweka hai matumaini ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao kwa mara ya kwanza tangu 2016-17 baada ya kupepeta Manchester United 3-1 mnamo Jumamosi ugani Emirates.

Brentford ambao wameshinda mechi tano kati ya sita zilizopita, sasa wanakamata nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 40 sawa na Brighton. Matokeo dhidi ya Spurs yaliwapa uhakika wa kusalia katika EPL msimu ujao huku zikisalia mechi tano pekee kabla ya kampeni zao za EPL muhula huu kutamatika rasmi.

Mechi dhidi ya Spurs ilimpa Eriksen jukwaa maridhawa la kuendeleza makali yake tangu arejee Uingereza kunogesha soka ya EPL baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa mechi iliyokutanisha Denmark na Finland kwenye fainali za Euro 2020.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 30 sasa anawaniwa pakubwa na Man-United watakaokuwa chini ya mkufunzi Erik ten Hag msimu ujao wa 2022-23. Eriksen ambaye mkataba wake na Brentfod unakatika mwishoni mwa muhula huu, alichezea Spurs mara 305 katika kipindi cha miaka sita na nusu.

Licha ya kufunga mabao 25 kutokana na mechi saba zilizopita za EPL, Spurs walikosa kuelekeza kombora lolote lililolenga shabaha langoni mwa Brentford. Ilikuwa mara yao ya nne kufanya hivyo msimu huu.

Chini ya kocha Antonio Conte ambaye ni raia wa Italia, Spurs kwa sasa wana kibarua kigumu dhidi ya Leicester City na Liverpool kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Arsenal mnamo Mei 12 katika mchuano utakaoamua nani ataungana na Man-City, Liverpool na Chelsea ndani ya orodha ya nne-bora katika EPL muhula huu.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Arsenal 3-1 Man-United

Leicester 0-0 Aston Villa

Man-City 5-1 Watford

Norwich 0-3 Newcastle

Brentford 0-0 Tottenham

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ijumaa, Aprili 29 ni sikukuu ya mapumziko Kenya kwa heshima...

Waislamu Mlima Kenya watoa wito Wakenya wadumishe upendo na...

T L