• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Ijumaa, Aprili 29 ni sikukuu ya mapumziko Kenya kwa heshima ya Kibaki – Matiang’i

Ijumaa, Aprili 29 ni sikukuu ya mapumziko Kenya kwa heshima ya Kibaki – Matiang’i

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya imetawaza Ijumaa, Aprili 29, 2022 kuwa Siku ya Mapumziko ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa ibada ya kumsindikiza Rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Mazishi ya Kibaki alisema kuwa siku hiyo imetengwa mahsusi kwa Wakenya kutoa heshima zao za mwisho kwa Kibaki.

Rais huyo wa tatu wa Jamhuri ya Kenya atazikwa nyumbani kwake eneobunge la Othaya, Nyeri katika hafla ya mazishi ya kitaifa, mnamo Jumamosi Aprili 30, 2022.

Ibada ya kitaifa ya wafu itafanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Michezo ya Nyayo jijini Nairobi.

Mwili wa mwendazake umehifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Lee, Nairobi.

Alifariki mnamo Ijumaa asubuhi, Aprili 22,2022 katika Nairobi Hospital ambako alikimbizwa baada ya kuzidiwa na ugonjwa.

“Serikali inatangaza Ijumaa, Aprili 29, 2022 kuwa Siku ya Mapumziko ili kumpa Rais Mwai Kibaki Mazishi ya Kiserikali,” Dkt Matiang’i akasema kupitia tangazo rasmi katika toleo la kipekee la Gazeti Rasmi la Serikali.

Dkt Matiang’i alisema kuwa hafla ya mazishi ya Kibaki itaendeshwa kwa taadhima na kanuni ya kijeshi.

  • Tags

You can share this post!

Usajili wa mitihani ya kitaifa 2022 kuanza Jumatano

Tottenham wapitwa na Arsenal baada ya kukabwa koo na...

T L