• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Waislamu Mlima Kenya watoa wito Wakenya wadumishe upendo na amani

Waislamu Mlima Kenya watoa wito Wakenya wadumishe upendo na amani

NA LAWRENCE ONGARO

JAMII ya Waislamu kutoka Mlima Kenya imewahimiza Wakenya wadumishe amani hasa wakati huu taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Sheikh Shaban Bakari, walisema kuna haja ya kila Mkenya kudumisha amani nchini kwa sababu ya “umoja wetu sote.”

Waislamu hao walipongeza mwaliko waliopokea wa hivi majuzi katika Ikulu ya Nairobi na Rais Uhuru Kenyatta.

Walisema Rais Kenyatta alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani hasa wakati huu tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Sheikh Bakari alisema jamii ya waislamu walichangisha takriban Sh17 milioni za kununua ambulansi itakayowasaidia Waislamu wanaohiji Mecca, nchini Saudi Arabia kama dharura ikitokea.

Rais alijitolea na kuchanga Sh5 milioni zitumike kununua ambulansi hiyo.

Kulingana na takwimu zilizotolewa, kuna idadi ya waislamu 600,000 waliochukua kura huku wakisema pia wana nafasi murwa ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura ifikapo mwezi Agosti.

Sheikh Bakari alisema wao kama waislamu wataketi chini halafu wajadiliane na baadaye watafanya uamuzi mwafaka ili kuchagua kiongozi wanayefikiria atadumisha amani na kuleta Wakenya wote pamoja.

“Bila shaka wakati ukifika tutazungumza kwa sauti moja,” alisema Sheikh Bakari.

Mwenyekiti wa Waislamu katika kaunti ya Kiambu, Imam Shuaib Mohamed, aliwahimiza walio na mali wawe wakarimu na kuwajali maskini kutokana na hali ya uchumi ilivyowabana Wakenya.

Alisema wakati wa janga la Covid-19 Wakenya wengi waliathirika na hadi sasa bado wengi hawajajitegemea ipasavyo.

Alisema Waislamu wako tayari kumuunga mkono kiongozi yeyote atakatechaguliwa na wapigaji kura.

“Sisi kama Waislamu ni watu wanaopenda amani na kwa hivyo hatungetaka kushuhudia machafuko yoyote hapa nchini,” alifafanua Imam Mohamed.

Naye mwekahazina wa chama cha waislamu cha Supkem mjini Nyeri, Sheikh, Nassor Mohamed, alitoa wito kwa vijana kudumisha amani na wasikubali kutumiwa vibaya na viongozi wakati huu wa kampeni za kisiasa.

“Viongozi wanastahili kuonyesha mwelekeo mwema kwa wananchi. Hatungetaka kushuhudia vurugu wakati huu wa kampeni,” akashauri Sheikh Mohamed.

Alieleza kuwa kila mwananchi ana nafasi yake ya kuishi kwa amani na kwa hivyo kila mmoja ana jukumu la kuonyesha upendo.

  • Tags

You can share this post!

Tottenham wapitwa na Arsenal baada ya kukabwa koo na...

Jalang’o ashinda tiketi ya ODM kuwania kiti cha...

T L