• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Tujiandae kwa Olimpiki za Paris 2024 sasa – Namcos

Tujiandae kwa Olimpiki za Paris 2024 sasa – Namcos

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Innocent “Namcos” Simiyu anataka timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande maarufu kama Shujaa, ianze kujiandaa kwa Olimpiki 2024 sasa hivi.

Katika mahojiano naye hapo Agosti 5, nahodha huyo wa zamani wa Shujaa alisema kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu katika kupata matokeo mema.

“Mashindano ya Olimpiki 2020 jijini Tokyo yalikuwa mazuri na pia kutufanya tufahamu kuwa bado tuko mbali katika kufikia kiwango cha kuwania medali. Hata hivyo, funzo kubwa tulilopata katika kampeni yetu ni kuwa tunafaa kuanza maandalizi ya makala yajayo ya Olimpiki hivi sasa,” alisema.

Simiyu, ambaye aliajiriwa na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) mnamo Septemba 2020 kwa kandarasi ya miaka miwili, alishuhudia vijana wake wakipoteza michuano yote ya makundi dhidi ya Amerika 19-14, Afrika Kusini 14-5 na Ireland 12-7 kabla ya kupiga Japan 21-7 katika nusu-fainali ya nambari tisa hadi 12 (mwisho).

Kenya kisha ililipiza kisasi dhidi ya Ireland zilipokutana katika fainali ya kuamua nambari tisa na 10 kwa kuichabanga 22-0.

Aidha, Namcos ameeleza kufurahia kuwa hali ya kawaida imeenza kurejea viwanjani baada ya Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby) kutangaza Agosti 4 kuwa Raga za Dunia zitaanza tena na duru ya Vancouver Sevens nchini Canada mnamo Septemba 18-19.

Duru hiyo ya kwanza tangu Vancouver Sevens mwezi Machi mwaka 2020, itafuatiwa na Edmonton pia nchini Canada mnamo Septemba 25-26.

“Ni kitu kizuri kwa sababu tunafurahia mambo yanarejea kuwa kawaida na wachezaji wanaweza kucheza mchezo wanaopenda,” alisema na kufichua kuwa wachezaji waliokuwa Olimpiki watapumzika kwa majuma mawili.

Wachezaji hao ni William Ambaka, Vincent Onyala, Herman Humwa, Collins Injera, Eden Agero, Billy Odhiambo, Nelson Oyoo, Andrew Amonde, Alvin Otieno, Daniel Taabu, Johnstone Olindi, Jeff Oluoch na Jacob Ojee. Nahodha Amonde alistaafu baada ya Olimpiki.

Shujaa ilirejea nyumbani kutoka Japan mnamo Agosti 1. Wachezaji ambao hawakusafiri wanaendelea na mazoezi katika uwanja wa KRU kwenye barabara ya Ngong Road jijini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 160 Githunguri wapata ufadhili wa Sh5 milioni

Spurs wataka Man-City iwape Sh24.9 bilioni kwa ajili ya...