• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Wanafunzi 160 Githunguri wapata ufadhili wa Sh5 milioni

Wanafunzi 160 Githunguri wapata ufadhili wa Sh5 milioni

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wapatao 160 kutoka eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, wanaotarajia kujiunga na Kidato cha Kwanza watanufaika na ufadhili wa Sh5 milioni.

Kati ya wanafunzi hao wanafunzi 40 watanufaika na ufaidhili kamili wa masomo huku waliosalia watapokea Sh20,000 kwa ufadhili huo.

Ufadhili huo unadhamiwa na hazina ya ustawi wa eneobunge la Githunguri kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), benki ya Equity, benki ya Family, Fresher Dairy na Wa Lydia Foundation.

Mpango huo unatoa ufadhili kwa wanafunzi werevu waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane wakijiandaa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Mgeni wa heshima kwenye hafla hiyo iliyofanyika MKU mnamo Alhamisi, Dkt Vincent Gaitho, ambaye ni pro-chansela, alipongeza hatua hiyo akisema ni njia moja ya kubadilisha mwelekeo wa wanafunzi hao kielimu.

“Matokeo mema ya ufanisi wenu yatanufaisha jamii na mwanafunazi mwenyewe, na kwa hivyo ni vyema kufanya bidii masomoni,” alisema Dkt Gaitho.

Alisema fedha za kutosha zinastahili kutengwa kutoka kwa serikali kupitia Hazina ya Kitaifa ili mpango wa wanafunzi kutoka shule za msingi hadi za upili uweze kufanikiwa.

Hata hivyo, alisema ukaguzi wa fedha hizo unastahili kuangaziwa kwa makini ili kusiwe na ufisadi katika mpango huo.

Kasisi Lawrence Kamere aliyehudhuria hafla hiyo aliwashauri wazazi wahamasishe wana wao kufuata maagizo yote ya kupunguza kuenea kwa Covid-19 hasa wakati huu ambapo wanafunzi wamerejea shuleni.

“Wanafunzi wanastahili kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba wanafuata sheria na masharti ya kuzuia kuenea kwa Covid-19,” alisema

Wanafunzi hao waliohudhuria hafla hiyo walishauriwa kujitahidi na kufanya bidii masomoni ili wajitegemee katika maisha ya baadaye.

You can share this post!

Mfanyabiashara anayeshtakiwa kujaribu kuua maafisa wawili...

Tujiandae kwa Olimpiki za Paris 2024 sasa – Namcos