• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Twaha Mbarak kuwania urais FKF

Twaha Mbarak kuwania urais FKF

Na JOHN ASHIHUNDU

Twaha Mbarak Ali raia wa ukanda wa Pwani amejitoza uwanjani kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi ujao wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Huku akiandamana na mgombeaji mwenza, Andrew Amukowa kutoka ukanda wa Magharibi, Twaha alitangaza habari hizo jijini Nairobi huku akiungwa mkono na wanasoka wastaafu wakiongozwa na Josephat Murila “Controller”.

Kadhalika waamuzi wastaafu, viongozi wa chama cha makocha wa kandanda na wawakilishi kutoka sehemu zote nchini waliahidi kumwuunga mkono. Mbali na Murila, wachezaji wengine wa zamani waliotangaza kumuunga mkono ni Douglas Mutua , Rickty Solomon, Mike Otieno, Peter Odero, Peter Ouma, Peter Lichungu na Mike Amwayi.

Twaha alisema uongozi wa kandanda inahitaji watu wapya, huku akisisitiza kwamba kundi lake ndilo lililo na watu wa aina hiyo. “Twaha na Amukowa watalewta mabadiliko ambayo Wakenya wameyasubiri kwa miaka mingi. Chini yetu, kutakuwa na usimamizi bora mpirani.

Tuko tayari kuleta pamoja washikaji dau tusaidiane kuinua mchezo huu ambao umedidimia. Tunahitaji kila mtu ili tufaulu.”Alisema afisi yake itahakikisha kuna usimamizi bora wa fedha za shirikisho ili kuvutia wafadhili zaidi, huku akiongoza kwamba atashirikiana na Serikali Kuu pamoja na ile ya kaunti kwa minajili ya kuinua mchezo huo kwa jumla.

Alisema vituo vya kunoa vipaji ni miongoni mwa mipango yake mara tu atakapotwaa uongozi, huku akiahidi kuweka viwanja vyote katika hali nzuri. Twaha alisema anaunga mkono hatua ya Waziri wa Michezo, Amina Mohamed pamoja na usimamizi wa sasa wa kamati ya muda ya Aaron Ringera ambayo imepewa jukumu la kusimamia shughuli za soka kwa miezi sita hadi viongozi wapya wachaguliwe.

“Tunataka kukarabati viwanja vyetu ili vifikie matakwa ya kimataifa na kuhakikisha timu ya taifa-Harambee Stars inapata usaidizi unaofaa ili turejee tena katika mashindano makubwa ya kimataifa kama Afcon na Kombe la Dunia,” alisema.

You can share this post!

Mukidza kuwa nahodha wa Kenya Simbas ikipepetana na...

Washukiwa wanne wakamatwa kwa kudaiwa kuiba nyaya za stima...

T L