• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ufaransa yateleza tena huku Uholanzi ikitamba katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022

Ufaransa yateleza tena huku Uholanzi ikitamba katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

WASHIKILIZI wa Kombe la Dunia, Ufaransa, walijikwaa tena katika kampeni za kufuzu kwa fainali za kipute hicho mnamo 2022 nchini Qatar baada ya Ukraine kuwalazimishia sare ya 1-1 mnamo Jumamosi jijini Kiev.

Mechi hiyo iliyompa fowadi wa Manchester United, Anthony Martial, fursa ya kufunga bao lake la kwanza ndani ya jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa katika kipindi cha miaka mitano.

Ilikuwa mechi ya tano mfululizo kwa Ufaransa kukabwa koo. Tangu wapepete Ujerumani 1-0 katika hatua ya makundi ya Euro 2020 mnamo Juni 15, Ufaransa waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Hungary mnamo Juni 19 kabla ya Ureno kuwabana kwa sare ya 2-2 mnamo Juni 23.

Hadi waliposhuka dimbani kumenyana na Ukraine, walikuwa wametoshana nguvu na Uswisi (3-3) na Bosnia-Herzegovina (1-1) katika mapambano ya Euro na kufuzu kwa Kombe la Dunia mfululizo.

Licha ya sare dhidi ya Ukraine, Ufaransa ya kocha Didier Deschamps ingali kileleni mwa Kundi D kwa alama tisa, nne zaidi kuliko Finland na Ukraine. Bosnia-Herzegovina na Kazakhstan wanashikilia nafasi mbili za mwisho kundini kwa alama mbili kila mmoja.

Ushindi dhidi ya Finland jijini Lyon mnamo Septemba 7, utawawezesha Ufaransa kufungua mwanya wa pointi saba ikizingatiwa kwamba Ukraine watasakata mchuano wao ujao wa kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Finland mnamo Oktoba 9.

Finland wataingia ugani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Kazakhstan katika mchuano uliopita.Martial aliyekosa kuwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Euro 2020 kutokana na jeraha la goti, alifunga bao la kwanza katika ngazi ya kitaifa baada ya mechi 29.

Goli lake lilifuta juhudi za kiungo Mykola Shaparenko wa Ukraine.“Hatuko katika hali shwari zaidi lakini tunapania kujinyanyua dhidi ya Finland na kurejea tunakostahili kuwa. Alama tatu katika mechi ijayo zitatusaidia kufanya hivyo,” akasema Deschamps.

Ukraine nao wamesajili sare katika michuano mitano iliyopita ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, ikiwemo miwili dhidi ya mabingwa mara mbili Ufaransa (1998, 2018).

Kwingineko, mshambuliaji matata wa Barcelona, Memphis Depay, alipachika wavuni mabao mawili na kuongoza Uholanzi kukomoa Montenegro 4-0 jijini Eindhoven. Ushindi huo ulipaisha Uholanzi hadi nafasi ya pili katika Kundi G kwa alama 10, moja pekee nyuma ya viongozi Uturuki waliopepeta Gibraltar 3-0.

Chini ya kocha Louis van Gaal, Uholanzi walifunga mabao mengine kupitia Cody Gakpo na nahodha Georginio Wijnaldum. Kikosi hicho kitaalika Uturuki jijini Amsterdam hapo kesho.

Hii ni awamu ya tatu kwa Van Gaal aliyejaza pengo la Frank de Boer mnamo Agosti, kuhudumu kambini mwa Uholanzi. Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 69 aliwahi kudhibiti mikoba ya Uholanzi mnamo 2000-2002 na 2012-2014 kabla ya kuyoyomea Uingereza kunoa Manchester United waliompiga kalamu mnamo 2016.

Mnamo 2014, Van Gaal aliongoza Uholanzi kukamilisha kampeni za Kombe la Dunia nchini Brazil katika nafasi ya tatu kabla ya kutua Man-United alikonyanyua Kombe la FA katika msimu wake wa mwisho ugani Old Trafford.

Tangu Van Gaal ajiuzulu mnamo 2014, timu ya taifa ya Uholanzi imejivunia huduma za wakufunzi saba tofauti wakiwemo Guus Hiddink, Danny Blind, Dick Advocaat na Ronald Koeman.

Katika matokeo mengine ya Jumamosi, chipukizi Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund alifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Norway dhidi ya Latvia.

Norway sasa wanajivunia alama 10, tatu kuliko Montenegro watakaovaana na Latvia hapo kesho.Croatia waliotinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 walipiga Slovakia 1-0 katika Kundi H na kupaa hadi nafasi ya pili kwa alama 10 sawa na viongozi Urusi waliocharaza Cyprus 2-0.

Slovenia walipepeta Malta 1-0 katika gozi jingine la kundi hilo.Denmark walitandika Faroe Islands 1-0 katika Kundi F lililoshuhudia Israel wakichabanga Austria 5-2 na Scotland wakipiga Moldova 1-0.

Serbia waliwapiku Luxembourg kwa 4-1 huku Jamhuri ya Ireland ikisajili sare ya 1-1 dhidi ya Azerbaijan katika Kundi A.

  • Tags

You can share this post!

Falcao arejea Uhispania kuchezea Rayo Vallecano baada ya...

Kinara wa Arsenal atetea matumizi ya fedha ya kikosi hicho...