• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:12 PM
Uholanzi, Uingereza na Ubelgiji wakamilisha maandalizi ya Euro kwa kushinda mechi za kirafiki

Uholanzi, Uingereza na Ubelgiji wakamilisha maandalizi ya Euro kwa kushinda mechi za kirafiki

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

UHOLANZI, Uingereza na Ubelgiji walikamilisha maandalizi ya Euro 2020 kwa kushinda michuano yao ya kujipima nguvu mnamo Jumapili usiku.

Uingereza wanaopigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa Euro mwaka huu, waliwapokeza Romania kichapo cha 1-0 huku Ubelgiji wakisajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Croatia ambao wataanza kampeni za Kundi D dhidi ya Uingereza mnamo Jumapili ugani Wembley. Uholanzi walizamisha chombo cha Georgia kwa mabao 3-0.

Kocha Gareth Southgate alitumia mechi kati yao na Romania kupima uwezo wa wanasoka watatu – Ben Godfrey, Ben White na James Ward-Prowse ambao hawakuwa katika kikosi chake cha awali cha masogora 26 kwa ajili ya Euro.

Aliyeridhisha zaidi kati yao ni beki wa Brighton, White, ambaye kwa sasa atakuwa kizibo cha Trent Alexander-Arnold wa Liverpool aliyepata jeraha la paja wakati wa mchuano wa kirafiki dhidi ya Austria mnamo Jumatano iliyopita jijini London.

White anatarajiwa kuwania nafasi ya kuchezeshwa kama beki wa kulia katika kikosi cha Uingereza licha ya ushindani mkali kutoka kwa Kieran Trippier wa Atletico Madrid, Kyle Walker wa Manchester City na Reece James wa Chelsea.

Wakicheza dhidi ya Romania, Uingereza walifunga bao la pekee kupitia Marcus Rashford aliyeweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi mweusi kuwahi kuvalia utepe wa unahodha kambini mwa Uingereza akiwa na umri wa miaka 23 na siku 218.

Pambano hilo lilikuwa la kwanza kwa kipa Sam Johnstone wa West Bromwich Albion kuwajibikia Uingereza na lilimpa kiungo na nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson, fursa ya kurejea ugani kwa mara ya kwanza tangu apate jeraha la kinena mnamo Februari.

Kwa upande wao, Ubelgiji walifunga bao lao dhidi ya Croatia kupitia Romelu Lukaku wa Inter Milan aliyeshirikiana na beki Jason Denayer wa Olympique Lyon.

Ubelgiji walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Ugiriki kuwalazimishia sare ya 1-1 Alhamisi iliyopita. Kikosi hicho kinashikilia nambari moja kimataifa kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kitafungua kampeni za Kundi B katika Euro dhidi ya Urusi mnamo Juni 12 kabla ya kupepetana na Denmark mnamo Juni 17 kisha Finland mnamo Juni 21.

Uholanzi wanaokamata nafasi ya 16 duniani, wanapigiwa upatu wa kusonga mbele zaidi kutoka Kundi C ambalo pia linajumuisha Austria, Ukraine na Macedonia Kaskazini.

Chini ya kocha Frank de Boer, Uholanzi walifunga mabao yao dhidi ya Georgia kupitia Wout Weghorst, Ryan Gravenberch na Memphis Depay aliyeshirikiana pakubwa na Frenkie de Jong na nahodha Georginio Wijnaldum. Wataanza kivumbi cha Euro dhidi ya Ukraine mnamo Juni 13 bila kujivunia huduma za beki Matthijs wa Juventus anayeuguza jeraha la goti.

Gozi dhidi ya Georgia lilimpa kipa mzoefu wa Ajax, Maarten Stekelenburg, jukwaa la kuchezea Uholanzi kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2016.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 38 amewahi pia kudakia Fulham, Southampton na Everton. Anatarajiwa kuwa tegemeo la Uholanzi katika Euro baada ya Jasper Cillessen wa Valencia kuugua corona.

You can share this post!

Corona: Uganda yasitisha kufunguliwa kwa shule

Pigo kwa timu ya taifa ya Uhispania baada ya corona kubisha...