• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Uhusiano wa Malkia Elizabeth, ‘pembe za ndovu’ jijini Mombasa

Uhusiano wa Malkia Elizabeth, ‘pembe za ndovu’ jijini Mombasa

NA JURGEN NAMBEKA

HUKU dunia nzima ikiomboleza kifo cha Malkia Elizabeth wa pili, aliyeaga dunia Alhamisi akiwa katika kasri la Balmoral, Scotland huko Uingereza, watalii wa kigeni na wa humu nchini waliozuru eneo la pembe za ndovu katika barabara ya Moi Avenue jijini Mombasa, walionekana kuelewa uhusiano wa pembe hizo na Malkia huyo.

Kulingana na afisa wa makavazi ya Kitaifa Bw Raphael Abdulmajid, kivutio hicho ni cha pili kuzuriwa na watalii baada ya Fort Jesus, kila wanapozuru jiji la Mombasa.

Kulingana na Bw Abdulmajid, viongozi wa eneo jiji la Mombasa walitaka kumkaribisha Malkia Elizabeth kwa njia ya kipekee alipokuwa katika safari yake nchini mnamo 1952.

“Viongozi wa hapa walitaka kuweka minazi kama ilivyokuwa utamaduni wa jamii za Pwani kuwakaribisha wageni. Kwa kutaka idumu zaidi viongozi hao waliamua kutumia mbao badala ya minazi hiyo ambayo huenda ingenyauka,” alisema Bw Abdulmajid.

Kulingana naye msimbo huo wa minazi iliyopitana, ambayo iliishia kufanana na pembe za ndovu, ulikuwa kwa barabara moja ila barabara ilipopanuliwa kuwa na njia mbili nyingine ikawekwa.

Hapo baadaye pembe hizo zilibadilishwa na kuundwa kwa chuma, marekebisho yakifanywa kila mara kuhakikisha pembe hizo ziko imara kila uchao.

“Malkia Elizabeth wa pili aliaga Septemba 8, na ni msimbo wa uhusiano mzuri baina ya Kenya na Uingereza. Mwaka wa 1952 Malkia alikuwa hapa na humu nchini ndiko alipopata habari za babake kuaga na akatawazwa Malkia. Ni vyema kupiga picha kwenye pembe hizi ila ni muhimu zaidi kufahamu historia iliyoko nyuma ya pembe hizi,” alisema Bw Yomi Adu.

Bw Adu hakuwa na ufahamu wa maana nyuma ya pembe hizo za ndovu, ila alifurahia alipoelezewa na mkazi wa jiji la Mombasa kuhusu lilikotoka.

Kwa mtalii mwingine kutoka Afrika Kusini Bi Anathi Tshale, alikuwa amepanga kuzuru Mombasa ila alikuwa amefanya utafiti wa Pembe hizo.

“Nilijifunza historia ya pembe hizi na ni sadfa kuwa wakati niliopanga kufika hapa kuziona umegongana na kifo cha Malkia huyo Elizabeth. Inanishtua kuwa ziliwekwa kumkumbuka ilhali si eti alikuwa mzuri hivyo,” alisema Bi Tshale.

Kwa mpigapicha Benson Ndung’u ambaye amekuwa akijitafutia kwa kunakili kumbukumbu za watalii wengi, ana historia ya pembe hizo na kila mara yeye huwajuza wanaozuru pembe hizo.

“Ni vizuri kuelezea wanaotembea huku kuhusu pembe hizi. Malkia alikuwa mtu mashuhuri na anayejulikana na watu wengi duniani na hata hapa Kenya. Naomba Mungu amuongoze katika safari yake,” alisema Bw Ndung’u.

Kwa wakazi wengine, umuhimu wa pembe hizi ama historia ya pembe zenyewe ni usiku wa kiza.

“Pembe hizi ziliwekwa hapa kuonyesha umaarufu wa ndovu na pembe zake. Hizi pembe ziliwekwa hapa kurembesha mji wetu,” alisema Bw Ndung’u.

Pembe hizo ziliwekwa kama ishara ya heshima kwa Malkia Elizabeth II kuzuru jiji la Mombasa.

Mnamo Februari 1952 Malkia Elizabeth alikuwa katika ziara yake humu nchini. Ni katika wakati uo huo alipotembelea maeneo mbalimbali ya nchi ya Kenya huku kukiwa na picha za kuhudhuria hata ibada katika kanisa mbalimbali ambako kumbukumbu ya Malkia huyo kuzuru nchi hii kuwepo.

  • Tags

You can share this post!

Ongwae aongoza viongozi kadhaa kujiunga na Ruto

Rais atangaza siku 4 za maombelezo kwa heshima ya Malkia

T L