• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Uwanja maarufu wa Maracana nchini Brazil sasa kuitwa Rei Pele kwa heshima ya jagina huyo wa soka

Uwanja maarufu wa Maracana nchini Brazil sasa kuitwa Rei Pele kwa heshima ya jagina huyo wa soka

Na MASHIRIKA

UWANJA maarufu wa Maracana nchini Brazil sasa utabadilishwa jina na kuitwa Rei Pele Stadium kwa heshima ya jagina wa soka katika taifa hilo, Edson Arantes do Nascimento.

Mpango wa kutekelezwa kwa mabadiliko hayo tayari umeidhinishwa na bunge la kitaifa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Edson Arantes do Nascimento ndilo jina kamili la mwanasoka huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 80 na Rei ni jina lililo na maana ya mfalme katika lugha ya Kireno.

Kilichosalia kwa sasa ni gavana wa jiji la Rio de Janeiro kutia saini pendekezo ambalo limeidhinishwa na bunge kabla ya jina la uwanja wa Maracana uliotumiwa kuandalia fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ujerumani na Argentina mnamo 2014 kubadilishwa rasmi.

Pele aliyeshindia Brazil mataji matatu ya Kombe la Dunia akiwa mchezaji, alifunga bao lake la 1,000 kitaaluma uwanjani Maracana mnamo 1969 akisakatia kikosi cha Santos dhidi ya Vasco da Gama.

Mbali na kutumiwa kuandalia fainali za Kombe la Dunia mnamo 2014, uwanja huo wa kihistoria nchini Brazil ulitumiwa pia kuandalia fainali za Kombe la Dunia mnamo 1950 na Olimpiki za Rio mnamo 2016.

Licha ya kuwa na uwezo wa kubeba mashabiki 78,838 pekee walioketi, zaidi ya mashabiki 200,000 waliwahi kuruhusiwa kuingia katika uwanja wa Maracana kushuhudia mechi ya fainali ya Kombe la Dunia iliyoshuhudia Uruguay ikiwabwaga Brazil mnamo 1950.

Japo unaitwa Maracana, uwanja huo uliitwa kwa heshima ya Mario Filho, mwanahabari aliyehamasisha shughuli za ujenzi wake katika miaka ya 1940. Maracana ni eneo ambalo uga huo umejengwa.

Pele aliwahi kufunga mabao 12 kutokana na mechi 14 za Kombe la Dunia na akatikisa nyavu za wapinzani mara 1,283 kutokana na mechi 1,363.

Pele ndiye mwanasoka wa pekee kufikia sasa kuwahi kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia. Alizaliwa katika familia maskini licha ya kwamba baba yake mzazi, Dondinho, aliwahi kuchezea mojawapo ya klabu maarufu za soka kutoka Kusini Mashariki mwa mji wa Minas Gerais, Brazil.

Mwaka mmoja baada ya kuchezeshwa na kikosi cha Santos mjini Sao Paolo, Pele alichezeshwa na timu ya taifa ya Brazil kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16 na akaongoza miamba hao kutia kapuni Kombe la Dunia baada ya kupepeta wenyeji Uswidi 5-2 kwenye fainali ya 1958.

“Mabao mawili niliyofunga kwenye fainali hiyo yalinipa umaarufu. Mashabiki walianza kuniita ‘Mfalme Mweusi wa Brazil’ akaeleza nguli huyo wa soka.

Pele alitupilia mbali ofa nyingi za kuchezea vikosi vya bara Ulaya. Alivalia jezi za Santos kwa muda mrefu kabla ya kujiunga na New York Cosmos ya Amerika mnamo 1975. Jagina huyo wa soka sasa anaishi na mkewe wa tatu, Marcia Cibele Aoki, 48, jijini Sao Paulo, Brazil.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mashabiki wa Samidoh sasa wamshauri ajichunge asipake tope...

Klopp afutilia mbali uwezekano wa kuwa kocha mpya wa timu...