• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Vincent Kompany na Mauricio Pochettino miongoni mwa wakufunzi wanaopigiwa upatu kupokezwa mikoba ya Chelsea

Vincent Kompany na Mauricio Pochettino miongoni mwa wakufunzi wanaopigiwa upatu kupokezwa mikoba ya Chelsea

Na MASHIRIKA

VINCENT Kompany ni miongoni mwa wakufunzi ambao wametiwa kwenye orodha fupi ya makocha wanaowaniwa na Chelsea.

Kompany ambaye kwa sasa anawanoa Burnley, Mauricio Pochettino na mkufunzi mwingine ambaye hajatajwa ni kati ya makocha wanaohusishwa na mikoba ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Luis Enrique ambaye aliwahi kunoa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, pamoja na mkufunzi wa zamani wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann, tayari wameondolewa kwenye orodha ya wakufunzi wanaohusishwa na uwezekano wa kutua uwanjani Stamford Bridge.

Wakurugenzi wa Chelsea, Laurence Stewart na Paul Winstanley wanaongoza mchakato wa kutafuta mkufunzi mpya wa Chelsea.

Chelsea almaarufu Blues, walimtimua kocha Graham Potter mwanzoni mwa Aprili baada ya kipindi kisichozidi miezi saba baada ya kichapo cha 2-0 kutoka kwa Aston Villa uwanjani Stamford Bridge. Matokeo hayo yaliacha Chelsea katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Kocha wa zamani wa Chelsea na Everton, Frank Lampard aliaminiwa fursa ya kushikilia mikoba ya Chelsea hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23 baada ya Potter kupigwa kalamu.

Kompany ambaye ni beki na nahodha wa zamani wa Manchester City, ameongoza Burnley kupanda ngazi kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) hadi EPL katika msimu wake wa kwanza wa ukufunzi ugani Turf Moor.

Kompany, 37, amebadilisha pakubwa mtindo wa kucheza kwa Burnley na kutua kwake Chelsea kutakuwa hatua kubwa kitaaluma.

Hadi alipoajiriwa na Burnley, Kompany alikuwa amenoa kikosi cha Anderlecht pekee (2019-2022). Mafanikio anayojivunia kambini mwa Burnley yaliwahi pia kumfanya ahusishwe na mikoba ya Tottenham Hotspur.

Chelsea walikuwa tayari wamezungumza na Nagelsmann aliyepigwa kalamu na Bayern Munich mnamo Machi 2023. Hata hivyo, inaaminika kuwa kulikuwa na suitafahamu na hisia mseto kuhusu utendakazi wa kocha huyo raia wa Ujerumani.

Pochettino ambaye ni raia wa Argentina, hajakuwa na kazi tangu atimuliwe na Paris St-Germain (PSG) mwishoni mwa msimu uliopita wa 2021-22.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 aliwahi kudhibiti mikoba ya Spurs kwa miaka mitano na kuongoza mahasimu hao wa Chelsea jijini London kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019.

Enrique alikuwa akihusishwa pakubwa na mikoba ya Chelsea ila amekosa kuunga orodha fupi ya mwisho baada ya mahojiano ya awali.

Chelsea kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la EPL na watakuwa wenyeji wa Brentford katika EPL mnamo Aprili 26, 2023.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wakora wavamia akaunti za Vyombo vya Habari na kuchapisha...

Europa League: AS Roma kuvaana na Bayer Leverkusen kwenye...

T L