• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Vivian Moraa: Msichana anayefyatuka unyoya kama Omanyala

Vivian Moraa: Msichana anayefyatuka unyoya kama Omanyala

NA PATRICK KILAVUKA

ALIWAKILISHA kanda ya Nairobi katika mashindano ya Michezo ya Riadha kwa Shule za Msingi kitaifa ambayo yaliandaliwa katika uga wa Ole Ntimama, Narok kama bingwa wa mbio za mita 100 na kikosi cha mita 4×100. 

Anazamia kukimbia kama kielelezo Ferdinand Omanyala ambaye ni bingwa Afrika na Jumuiya ya Madola, na ambaye hata juzi alinyakua taji la Absa Kip Keino Continental Tour ugani Kasarani mnamo Jumamosi iliyopita kwa muda wa sekunde 9.84.

Vivian Moraa,13, ni mwanafunzi wa gredi ya saba shule ya msingi na World Hope Academy, Kawangware, Nairobi.

Yeye ni kitinda mimba katika familia ya watoto watatu wa Bw Leonard Omwenga na Bi Eunice Khavai.

Alianza mbio akiwa gredi ya pili ambapo alikuwa na anaelekezwa na mwalimu wake Veronicah Otieno.

Anasema alikuwa anamhimiza kuendelea kushiriki katika michezo kila uchao kama njia ya kukuza talanta na kujiimarisha afya.

Hata hivyo, alijiunga pia na mradi wa Awana ambao uliendelea kumchochea zaidi kujikuza kispoti.

Kujiandaa mwaka huu kwa mashindano ya Michezo ya Riadha Shule za Msingi, anasema alijifunga kibwebwe akiamini kwamba, atafika kitaifa majaliwa.

Mwanafunzi na mwanariadha Vivian Moraa akifanya mazoezi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Dua yake ilijibiwa pale ambapo alinogesha mbinu za mchezo huu kwa kukimbia mbio za umbali wa mita 100.

Katika mashindano ya Zoni ya Riruta yaliyoandaliwa Kawangware, aliibuka nambari wani kwa kusajili muda bora wa sekunde 11.80.

Alipanda ya Kaunti ndogo ya Dagoretti Mashariki na kuwa kidedea kwa muda wa sekunde 11.96 ambayo yaliandaliwa shule ya sekondari ya Dagoretti High.

Baada ya kujifua zaidi chini wa kocha  Geoffrey Wesonga, mwalimu wa michezo shuleni Raymond Shirandula na wadau  wengine shuleni, alipata muda bora zaidi katika mita 100 wa sekunde 12.60 katika mashindano ya Jimbo la Nairobi yaliyofanyika shule ya msingi ya Moi Forces, Nairobi.

Alichaguliwa kupeperusha bendera ya jimbo la Nairobi kitaifa.

Mtimkaji chipukizi Vivian Moraa wa Shule ya Msingi ya World Hope Academy akionyesha cheti cha ushindi ambacho alituzwa katika mashindano ya Michezo ya Riadha ya Shule za Msingi kanda ya Nairobi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Alipambana ukucha kwa jino, japo aliibuka wa saba bora kwa muda sekunde 12.96 kitaifa.

Alishiriki pia katika kikosi cha mbio za kupokezana vijiti za 4×100 Kanda ya Nairobi na kumaliza saba bora kitaifa kwa muda waka sekunde 13.76.

Alituzwa cheti cha ushindi mbio za 100 kanda ya Nairobi na vyeti vya kushiriki mita hizo na 4×100 kupokezana vijiti kitaifa.

Mwanariadha chipukizi Moraa anasema alikuwa anafanya mazoezi kila siku kuimarisha misuli.

Pia, alikuwa anajaribu kadri awezavyo kujiepusha na kukula vyakula vyenye mafuta mengi kwa kuzingatia lishe bora.

Changamoto yake ilikuwa kukimbia bila viatu vya kukimbia lakini baada ya kufanya vizuri, shule ilijitolea kumnunulia.

Hapo ndipo, alipata mori kutokana na utambuzi wa juhudi zake katika mchezo huo.

Katika masomo, mwalimu wake Moses Ayodi anasema ni mwanafunzi ambaye anapenda masomo na anapata alama juu.

Mwanariadha chipukizi Vivian Moraa wa Shule ya Msingi ya World Hope Academy akionyesha vyeti vyake akiwa na mwalimu wake Moses Ayodi (kulia), kocha wake Geofrey Wesonga na mwalimu wa michezo shuleni Raymond Shirandula (kushoto). PICHA | PATRICK KILAVUKA

Mbali na kujikasa masomo akinuia kusomea uhandisi wa maroboti huku  akipania  kuwa mwanariadha.

Mtimkaji Moraa anadokeza kwamba, anayachota mambo mengine kuhusu riadha kupitia mitandao ya kijamii kama njia ya kujua jinsi wanariadha wengine wanavyojiimarisha.

Kama hasomi wala hashiriki riadha, mkimbiaji huyu hucheza soka au mpira wa vikapu.

Ushauri wake ni kwamba, ukitaka kuwa mkimbiaji, anza pole pole, jitume na utafika ngazi za juu.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto akariri kuendelea kupambana na ufisadi

Bajeti kusomwa Juni 15

T L