• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Wakenya Nancy Cherono, Jelagat wavuna vinono Valencia Marathon

Wakenya Nancy Cherono, Jelagat wavuna vinono Valencia Marathon

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Nancy Jelagat na Lawrence Cherono walidumisha utawala wa Kenya kwenye mbio za Valencia Marathon hadi miaka miwili baada ya kutwaa mataji na kutuzwa Sh9.5 milioni na Sh6.3 milioni mtawalia nchini Uhispania hapo jana.

Jelagat, ambaye muda wake bora katika mbio hizo za kilomita 42 ulikuwa saa 2:36:22, aliuimarisha kwa karibu dakika 19 alipokata utepe kwa 2:19:31. Alifuatwa kwa karibu na Waethiopia Etagegne Woldu (2:20:16), Beyenu Degefa (2:23:04) na Rahma Tusa (2:23:20).

Wakenya Dorcas Tuitoek (2:24:54) na Bornes Chepkirui (2:25:37) waliridhika na nafasi ya nane na 11 mtawalia. Mtanzania Failuna Matanga alikamata nafasi ya 17 (2:27:58). Cherono, ambaye alimaliza Valencia Marathon 2020 katika nafasi ya pili, alitawala makala haya ya 41 kwa saa 2:05:12.

Muethiopia Chalu Deso (2:05:16) na Wakenya Philemon Kacheran (2:05:19) na Geoffrey Kamworor (2:05:23) waliridhika na nafasi tatu zilizofuata mtawalia. Mtanzania Gabriel Geay (2:06:10) alimaliza nafasi ya nane.Makala haya yalivutia washiriki 16,000.

Jelegat alizawadiwa Sh9.5 milioni kwa kumaliza kilomita 42 chini ya saa 2:20:00 naye Cherono kati ya 2:04:30 na 2:06:00. Aidha, mtimkaji Michael Githae ni Mkenya wa kwanza kushinda mbio za Fukuoka Marathon nchini Japan katika kipindi cha miaka sita.

Alifanya hivyo jana akinyakua taji kwa saa 2:07:51, muda ambao ni wake mpya bora baada ya kufuta ule wa 2:08:17 aliotimka akimaliza Fukuoka Marathon katika nafasi ya nne mwaka 2020.Bingwa huyo wa Shizuoka Marathon mwaka 2017 amefuatwa kwa karibu na Kyohei Hosoya (2:08:16), Mkenya James Rungaru (2:08:25), Shohei Otsuka (2:08:33) na Ryu Takaku (2:08:38) katika nafasi tano za kwanza.

Daisuke Uekado (2:08:56), Kohei Futaoka (2:09:14), Masaya Taguchi (2:09:35), Toshiki Sadakata (2:10:31) na Takuma Kumagai (2:10:41) wamekamilisha mduara wa 10-bora.

Bingwa wa Boston Marathon 2018 Yuki Kawauchi na mshindi wa Hong Kong Marathon 2013 Ser-Od Bat-Ochir ni baadhi ya majina makubwa yaliyobwagwa na Githae. Wakenya wengine ambao wamewahi kushinda Fukuoka Marathon ni Jackson Kabiga (1998), Samuel Wanjiru (2007), Josephat Ndambiri (2011), Joseph Gitau (2012), Martin Mathathi (2013) na Patrick Makau (2014 na 2015).

You can share this post!

Masikitiko Gor ikibanduliwa Caf nyumbani

Mombasa Elite yailaza Coastal Heroes 1-0 ligi ya NSL

T L