• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Wanakarate wa Zetech kupandishwa gredi

Wanakarate wa Zetech kupandishwa gredi

Na LAWRENCE ONGARO

WANAKARATE wapatao 12 wa chuo cha Zetech mjini Ruiru, wanajiandaa vilivyo ili kupandishwa gredi ya mishipi tofauti.

Kocha wa kikosi hicho kinachofahamika kama Sensei, Bw Martin Ndegwa, amesema kuwa tayari anawapa mazoezi makali vijana hao ili wawe makini na staili za kumite na kata ambazo ni muhimu wakati wa majaribio hayo.

Alieleza mwishoni mwa mwezi Januari 2022, kikosi hicho kimejiwasilisha mjini Thika kwa majaribio ya kupandishwa gredi ambapo baadhi yao wamewania kutuzwa mishipi ya manjano, kijani kibichi, na hudhurungi.

Alieleza kuwa kati ya wanakarate hao kuna wanaume saba na wanadada watano ambao wamejitolea kuona ya kwamba wanapiga hatua katika kiwango kingine.

“Baadhi yao pia wanatarajia kunoa makali yao ili kushiriki katika mashindano yajayo ya vyuo vikuu yanayodhaminiwa na Shirikisho la Spoti la Vyuo Vikuu (KUSF),” alifafanua kocha huyo.

Alieleza kuwa mashindano hayo yameratibiwa kung’oa nanga mwanzoni wa mwezi wa Februari 2022.

Anatarajia mashindano hayo yatakuwa mwanzo wa kuwainua vijana wake katika kiwango kingine.

“Msimu huu wa Januari 2022, tumezamia mazoezi kabambe ili kuona ya kwamba vijana wa Zetech wanajitambulisha katika ramani ya mchezo wa karate, kitaifa na kimataifa,” alieleza kocha huyo.

Kocha huyo anataka kuona kila mchezaji ana ujuzi wa staili ya kumite na kata.

Mnamo mwezi Disemba 2021, timu ya karate ya Zetech ilishinda mashindano ya JKUAT Karate Championship, kwa kuibuka ya kwanza kwa kuzoa dhahabu nne, fedha moja, na shaba moja.

Klabu ya Zetech ni miongoni mwa vikosi ambavyo vinavuma kutokana na wachezaji wake kumakinika michezoni.

“Msimu huu nitafanya juhudi kuona ya kwamba wanachuo wengi wanajiunga na mchezo huo ili kuwa wanakarate stadi,” alifafanua kocha huyo.

Kocha huyo anataka kuona ya kwamba msimu huu klabu ya Zetech inaorodheshwa miongoni mwa timu hodari.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge kurejea bungeni kesho kujaribu kuokoa jahazi la...

Mwanaharakati aliyezima BBI sasa kugombea useneta Migori

T L