• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Wanaraga wa Shujaa wapangiwa mechi zaidi za kirafiki barani Ulaya

Wanaraga wa Shujaa wapangiwa mechi zaidi za kirafiki barani Ulaya

Na CHRIS ADUNGO

WANARAGA wa timu ya taifa ya Shujaa wamepangiwa mechi tatu za ziada za kirafiki kwa minajili ya kujifua kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan kuanzia Julai 2021.

Kikosi hicho tayari kimeratibiwa kupimana nguvu na Ufaransa na Uhispania mnamo Februari 2021. Wakiwa katika mataifa hayo, Shujaa watavaana pia na vikosi vya New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa.

Kwa mujibu wa Eric Ogweno ambaye ni meneja wa timu ya Shujaa, Shirikisho la Raga Duniani (WR) limepania kuvipa vikosi ambavyo tayari vimefuzu kwa Olimpiki fursa nyingi za kujifua vilivyo kwa kampeni hizo za haiba kubwa.

Ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusu michuano hiyo ya ziada ya kupimana nguvu, Ogweno amesisitiza kwamba mechi hizo zitachezewa katika mataifa mawili ya bara Ulaya kati ya Aprili na Juni 2021.

Michuano hiyo inatarajiwa kupiga jeki maandalizi ya Shujaa ikizingatiwa kwamba duru za Hong Kong na Singapore kwenye kivumbi cha Raga ya Dunia zilizokuwa zifanyike Oktoba tayari zimeahirishwa. WR imefichua pia uwezekano wa kufutilia mbali duru za Vancouver (Canada) na Los Angeles (Amerika) ambazo zimepangiwa kufanyika Machi. Hii ni baada ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya Covid-19 katika mataifa hayo mawili.

Ogweno ameshikilia kwamba mataifa yatakayoandaa mechi hizo yatafichuliwa na WR kufikia mwisho wa wiki ijayo.

“Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) linawasiliana mara kwa mara na WR kuhusu mpangilio wa mechi hizo na kuhusu masuala ya usafiri ikizingatiwa ukali wa kanuni zilizopo kwa sasa katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya Covid-19,” akasema.

Shujaa walianza mazoezi mnamo Novemba chini ya uzingativu wa masharti makali ya Wizara ya Michezo na ile ya Afya kuhusu jinsi ya kukabiliana na virusi vya corona.

Chini ya kocha Innocent Simiyu, wanaraga hao wa Shujaa walirejelea mazoezi mnamo Januari 6 baada ya likizo fupi ya Krismasi na Mwaka Mpya huku wakijizatiti kwa michuano ya Ufaransa na Uhispania.

Kati ya wachezaji wote walioitwa kambini mwa Shujaa, wa pekee ambaye hakurejea ni nyota wa Nondescripts, Oscar Dennis aliyepata jeraha baya la mguu baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani mnamo Novemba. Hata hivyo, amerejea nchini kutoka Afrika Kusini alikofanyiwa upasuaji na anatazamiwa kusalia mkekani kwa zaidi ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

You can share this post!

Hofu Lamu kufuatia ongezeko la vijana wanaotumia dawa za...

Sampdoria wapiga Inter Milan breki kali katika Ligi Kuu ya...