• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Wanatenisi wa Kenya waanza mazoezi ya uwanjani baada ya matokeo mazuri ya vipimo vya corona

Wanatenisi wa Kenya waanza mazoezi ya uwanjani baada ya matokeo mazuri ya vipimo vya corona

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya tenisi ya wanaume ya Kenya ya Kombe la Davis la Afrika Kundi la Tatu imepokea matokeo yake ya virusi vya corona mnamo Agosti 9 yanayoonyesha hakuna aliye na virusi hivyo.

Vijana wa kocha Francis Rogoi walifanyiwa uchunguzi huo baada ya kuwasili nchini Misri hapo Agosti 8 na kupokea matokeo yao mnamo Agosti 9.

“Sisi sote tumepatikana bila virusi hivyo. Hata hivyo, masharti ya mashindano yanasema kila mtu atakuwa akipimwa mara kwa mara virusi hivyo ili kuhakikisha mashindano ni salama,” Rogoi alieleza Taifa Leo katika mahojiano ya simu kutoka jijini Cairo ambako mashindano hayo ya mataifa saba yataandaliwa kutoka Agosti 11-14.

Alifichua kuwa Kenya ilifanya mazoezi yake ya kwanza Jumapili jioni, lakini ya kunyoosha misuli kabla ya kuwa na vipindi viwili vya mazoezi ya uwanjani Smash hapo Jumatatu.

Kikosi cha Kenya kinajumuisha wachezaji Ismael Changawa, Kevin Cheruiyot, Albert Njogu, Ibrahim Kibet na Derrick Ominde.

Rais wa Shirikisho la Tenisi Kenya James Kenani (Kiongozi wa Msafara), Rose Wanjala (meneja wa timu) na Philomena Minoo (mnyooshaji misuli na daktari) na maafisa kutoka serikali Charles Thumbi na Cynthia Adhiambo, walisafiri na timu hiyo.

Mataifa yatakayoshiriki mashindano hayo ya kuwania tiketi ya kupandishwa daraja hadi mashindano ya muondoano ya dunia ni Algeria, Benin, Misri, Ghana, Msumbiji na Rwanda.

Droo itafanywa Agosti 10 jijini Cairo. Timu tatu zitakazofanya vibaya pia zitashushwa ngazi kushiriki Kundi la Nne la Afrika.

You can share this post!

Polisi wapigana mmoja akimlaumu mwingine kwa kujisaidia...

Corona yavuruga mipango ya vikosi siku chache kabla ya...