• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wanyonyi akung’uta Mandonga ‘Mtu Kazi’

Wanyonyi akung’uta Mandonga ‘Mtu Kazi’

NA CHARLES ONGADI

BONDIA Daniel Wanyonyi hatimaye alilipiza kisasi kwa kumshinda Karim ‘Mtu Kazi’ Mandonga wa Tanzania katika pigano lisilo la kuwania taji ukumbini Sarit Centre Expo, Nairobi mnamo Jumamosi usiku.

Ni pigano lililosubiriwa kwa hamu na mashabiki, hasa baada ya Mandonga kumkomoa Wanyonyi kwa njia ya TKO katika pigano la kwanza Januari 14 mwaka huu.

Mara hii Mandonga alishindwa kutamba na ngumi yake mpya ya ‘kinguki’ kutoka nchini Urusi, ambayo anaamini ni ya kutoboa na kulemaza.

Katika pambano hilo la uzani wa Lightheavy, Mandonga alianza kwa mashambulizi makali ila hakulenga sawa ngumi zake.

Wanyonyi aliwaka moto raundi ya tano akimdhibiti Mandonga kwa ngumi za tumbo na mbavu zilizomfanya kujikunja.

Bingwa wa zamani wa taji la Afrika (ABU), Wanyonyi, aligeuka simba marara katika raundi ya sita na 10.

Ni mashambulizi yaliyomwacha Mandonga akipepesuka na kudondoka chini mara mbili katika raundi hizo. Ikamlazimu refa Julius Odhiambo kumhesabia hadi 10 kabla ya kumruhusu kuendelea na pigano.

Marefa wote watatu George Athumani, Wycliffe Marende na Leonard Wanga walimpa Wanyonyi ushindi wa 100-88, 100-88 na 100-80, mtawalia.

Mandonga alikubali kushindwa. Alimpongeza Wanyonyi kwa ushindi na pia kuomba pigano jingine.

Wanyonyi alikiri ushindi huo ulimpa fahari tele na ni ishara ya kurudia ubora wake wa kale.

“Sikufanya mazoezi ya kutosha katika pigano letu la kwanza, lakini Mandonga sasa ametambua mimi ni nani,” akasema Wanyonyi anayetamani pigano la marudiano kumfunza tena adabu mpinzani huyo.

Kwingineko, kocha mkuu wa timu ya taifa ya ndondi Hit Squad, Benjamin Musa, ameahidi kuimarisha idadi ya medali katika mashindano ya Afrika jijini Yaounde, Cameroon mnamo Julai 26 hadi Agosti 6.

Katika mashindano ya mwaka jana jijini Maputo, Msumbiji, Kenya ilimaliza ya 12 kati ya nchi 18 zilizoshiriki.

Hit Squad walizoa medali nne; tatu za fedha na moja ya shaba.

  • Tags

You can share this post!

Afueni bei ya mahindi ikitarajiwa kushuka msimu wa uvunaji

Gavana Wanga alia kupokonywa mlinzi

T L