• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
PAUKWA: Ndovu kabomoa nyumba, majirani wamsaka Tundu

PAUKWA: Ndovu kabomoa nyumba, majirani wamsaka Tundu

NA ENOCK NYARIKI

TUNDU alipoona maisha yake yamo hatarini, alichupa kupitia dirishani na kujichoma kwenye migomba.

Bahati yake ni kuwa, shati alilolivua na kulitupa chini liliyapumbaza yale madume ya ndovu yakadhani kuwa ni Tundu mwenyewe aliyejikwaa na kuanguka.

Katika mbala mwezi, ndovu walilikanyagakanyaga shati la Tundu na kulizika mchangani. Kisha, yalilitutia udongo na kukata majani ya mgomba na kuyarusha juu ya udongo.

Wakati hayo yakiendelea, kundi jingine la ndovu upande wa chini wa shamba lilinusa harufu ya Tundu na kutimua mbio ndani ya migomba likimfuata.

Tundu aliwachengachenga ndovu na kutokomea kwenye msitu ulioweka mpaka baina ya shamba lao na Mto Nungunungu. Aliuparamia mti mrefu na kutulia tuli baina ya majani.

Asubuhi, shamba la Bwana Farijala lilikuwa mfano wa uwanja uliotumiwa kwa mazoezi ya vita. Nyumba ya msonge ya Tundu sasa ilikuwa imegeuka vifusi.

Mikungu ya ndizi ilikuwa imeangushwa ovyo baada ya ndovu kula kifu yao. Mabonge ya kinyesi na nyayo zilionyesha wazi adui aliyekuwa amelivamia shamba.

“Yuko wapi Tundu!’’Bwana Farijala alimwuliza mkewe kwa kimako kana kwamba usiku uliotangulia hawakuwa pamoja tena katika kitanda kimoja.

Farijala alipiga mbiu ya mgambo majirani wakaja kumsaidia kumtafuta Tundu.

Kwenye upembe mmoja wa shamba, waliona tilivyogo iliyokuwa imesababishwa na ndovu. Kwenye mshumbi wa mchanga ambalo walikuwa wameututia ulijitokeza upindo wa shati la Tundu. Moyo wa Bwana Farijala uling’oka.

(HADITHI ITAENDELEA)

You can share this post!

Washikadau wa soka waunga Namwamba kuongea na FIFA

Msasa wa mawaziri umekamilika, macho sasa yaelekezwa kwa...

T L