• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Watford wahitaji alama nne pekee kutokana na mechi tatu zilizosalia ili kurejea EPL kwa msimu wa 2021-22

Watford wahitaji alama nne pekee kutokana na mechi tatu zilizosalia ili kurejea EPL kwa msimu wa 2021-22

Na MASHIRIKA

WATFORD wanahitaji alama nne pekee kutokana na mechi nne zijazo za Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) ili kupanda ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao wa 2021-22.

Hii ni baada ya kikosi hicho kilichoteremshwa daraja kutoka EPL mwishoni mwa muhula wa 2019-20, kuwapokeza Norwich ambao ni viongozi wa jedwali Championship kichapo cha 1-0 mnamo Jumanne usiku.

Kipa Tim Krul wa Norwich ambao tayari wamepanda ngazi kunogesha EPL msimu ujao, alifanya kazi ya ziada ya kupangua makombora matatu mazito kutoka kwa mafowadi Ismaila Sarr na Ken Sema wa Watford.

Ilikuwa hadi dakika ya 57 ambapo Dan Gosling alifungia Watford bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo baada ya kukamilisha krosi ya Joao Pedro.

Norwich almaarufu The Canaries wangalitawazwa mabingwa wa taji la Championship muhula huu iwapo wangaliwacharaza wageni wao Watford katika mchuano huo.

Ingawa Mario Vrancic alipata nafasi kadhaa za kuwafungia Norwich bao, fataki za fowadi huyo zilidhibitiwa vilivyo na kipa Daniel Bachmann.

Watford ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini, wanahitaji alama nne zaidi kutokana na mechi tatu za mwisho za msimu huu ili kupanda ngazi baada ya Brentford kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Cardiff nao Swansea City kupigwa 1-0 na Queens Park Rangers.

Norwich City walipandishwa ngazi kushiriki EPL kwa mara ya tano baada ya washindani wao wakuu katika Championship – Brentford na Swansea kutoshinda mechi zao za wikendi iliyopita na hivyo kujiweka katika nafasi ya kutoweza kufikia Norwich ya kocha Daniel Farke kileleni.

Norwich wanarejea EPL mwaka mmoja pekee baada ya kushushwa ngazi kwenye kivumbi hicho mnamo 2019-20. Norwich wamepanda ngazi kushiriki EPL mapema sana kwenye kampeni za Championship tangu 2004.

Katika kampeni za EPL mnamo 2019-20, Norwich walipoteza jumla ya mechi 13 kati ya 15 za mwisho na wakateremshwa ngazi hadi Championship baada ya msimu mmoja pekee kwenye kivumbi cha Ligi Kuu.

Japo vikosi huwa vigumu kwa vikosi vinavyoshuka ngazi kwenye EPL kurejea haraka kunogesha kivumbi hicho, Norwich walisalia watulivu na wakajenga imani kwa kocha wao Farke huku wakidumisha idadi kubwa ya wanasoka waliowategemea kwenye EPL mnamo 2019-20.

Ingawa walijizolea alama nne pekee kutokana na mechi nne za ufunguzi wa kipute cha Championship, Norwich walipaa hadi kileleni mwa jedwali baada ya kushinda Middlesbrough katika mchuano wao wa 12 mnamo Novemba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Klabu zote sita za EPL zilizokuwa zimejiunga na European...

Dennis Waweru atangaza mchakato wa BBI kutamatishwa kabla...