• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
‘Aliyemzika’ Dedan Kimathi asimulia shujaa alivyosalitiwa

‘Aliyemzika’ Dedan Kimathi asimulia shujaa alivyosalitiwa

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA kuna jina ambalo huheshimika zaidi katika jamii ya Agikuyu, ni lile la Dedan Kimathi ambaye alikamatwa na wakoloni akiwa msituni kupambania uhuru wa taifa hili na ambapo aliishia kunyongwa asubuhi ya Februari 18, 1957.

Ni nyumba chache sana ambazo hazina picha ya Kimathi ukutani na umaarufu wake umekuwa wa kupokezanwa kwa vizazi.

Ushahidi wa umaarufu wake ni kuwa wiki iliyopita wale vijana wanaokuwa na rasta Jijini Nairobi na wanaojifahamisha kuwa Muungano wa Wafanyabiashara wa Rasta, na ambao hukisiwa kuwa ni “jeshi la jamii ya Agikuyu”, wote wakiwa ni wa kuzaliwa ‘hivi majuzi’ walijitokeza hivi majuzi kwa mjane wa Kimathi anayeugua, Bi Mukami Kimathi kumjulia hali.

Kimathi anakubalika kuwa angeishi kushuhudia taifa likipata Uhuru wa kujitawala, basi bila shaka ndiye angeibuka kuwa rais wa kwanza wa taifa hili.

Wanamuziki wengi wa jamii hiyo ya Agikuyu imetunga nyimbo ambazo zimebakia kuwa maarufu eneo hilo kuhusu Kimathi kama shujaa wa kijamii na wa mapambano ya Maumau kuhusu uhuru wa taifa.

Kunao ambao huashiria kuwa uhasama mkuu kati ya aliyeishia kuwa rais wa kwanza, hayati Mzee Jomo Kenyatta na Kimathi ndio uliishia kusalitiwa kwa Kimathi na akakamtawa ndio aondoe jam ya kimamlaka ambapo Uingereza na wakoloni wake walikuwa wakimpendelea Kenyatta atwae uongozi.

Ni katika hali hiyo ambapo kila mwaka ni lazima kuzuke mjadala kuhusu kifo cha Kimathi, alizikwa wapi na lini mwili wake utatolewa kwa jamii hiyo iuzike kwa heshima.

Wale wajasiri wa kimaoni husema kuwa serikali ya hayati mzee Kenyatta haingejituma kusaka mabaki hayo na iyape mazishi ya heshima kwa kuwa ndani ya nafsi yake alijua kuwa Kimathi katika uhaio wake na mauti yake alibakia kuwa maarufu zaidi kuliko serikali.

Inasemwa kuwa ndipo siasa hizo za kukataa katakata kutoa mabaki hayo ya Kimathi kwa jamii zilianzia mwaka wa 1963 Kenyatta akiingia ikulu kuanza huduma kama rais wa taifa huru.

Wengine hata hudai kuwa hayati Kenyatta hakuwa mpiganiaji Uhuru bali alikuwa mradi tu wa Uingereza wa kutoa utawala kwa Mkenya asili lakini akisalia kuwa na usemi ambao hadi leo hii, Wakoloni hao wanashikilia vipande vikubwa vya ardhi ya Mkenya licha ya ukombozi ukiwa na mada ya kupata uhuru na mashamba.

Kimathi alizaliwa Oktoba 31, 1920 katika kijiji cha Thenge kilichoko eneo bunge la Tetu, Kaunti ya Nyeri.

Alikuwa wa ukoo wa Ambui katika jamii hiyo, ukoo ambao unafahamika kwa kuwa na watu wengi wa hasira ya kasi na ambao ukizozana nao, kaa mbali sana nao hasa wakati wako karibu na kifaa kinachoweza kutumika kama silaha.

Mweledi wa Kimombo 

Ameorodheshwa kama aliyejiunga na shule ya msingi ya Karuna-ini ambapo aliibuka mweledi wa kuongea lugha ya Kiingereza aliyosema ni ya kumfaa katika kuhimiza wakoloni Wazungu waondoke Kenya Mwaafrika ajitawale.

Alijiunga kwa muda na shule ya upili ya Tumutumu na ambapo alijiondoa baada ya kudai kuwa ukoloni wa walimu wazungu haukuwa ukimwendea vyema.

Aliingia katika jeshi la Uingereza miaka ya 1940 lakini akaondoka pia huku hadi sasa ikidhihirika wazi hakuzaliwa kusikizana na Wakoloni.

Mwaka wa 1951 alijiunga rasmi na wapiganaji wa Mau mau baada ya kutambulika kuwa alichukia wakoloni na alikuwa shujaa wa kutaka uhuru wa mtu mweusi.

Aliteuliwa kuwa katibu Mkuu wa wapiganaji hao katika tawi la Thomson Fall na akaibuka kuwa mpenda nidhamu na utiifu kwa Mau Mau na ambapo anasemwa kuwa mwandalizi kiapo tosha wa wakati huo.

Mwaka wa 1951 alikamatwa na Wakoloni lakini askari weusi waliokuwa ndani ya kikosi cha usalama katika hali ya kutekeleza ujasusi wa kufaa Mau Mau walimsaidia kuhepa.

Mwaka wa 1953 aliunda jeshi thabiti eneo la Mlima Kenya, akiliita Kenya Defence Council (KDC) ambapo kazi ya hilo jeshi ilikuwa kushirikisha mikakati ya mapambano eneo hilo.

Ndani Kamiti

Oktoba 1956 alitiwa mbaroni na katika jela la Kamiti lililoko Kaunti ya Nairobi, akanyongwa kwa kamba hadi akafa.

Kifo hicho hukera wengi sana ambao wamekuwa wakifuatilia historia ya Mau Mau na ni hali ambayo hata kwa wale wamesambaziwa kasumba hiyo ya uzalendo wa kukomboa nchi, hata wakiwa wa umri wa ujana wa jana, hutiririkwa na machozi.

Huku siasa za kutolewa kwa mabaki ya Kimathi yazikwe kiheshima, sio tu mambo na kujenga mnara katikati mwa jiji ukiwa na kinyago cha kufanana naye, Shujaa mmoja wa vita vya Mau Mau Geoffrey Karitu Maraga kutoka Kaunti ya Nyandarua amekuwa akisema anajua mahali ambapo Kimathi alizikwa.

Yeye hukiri kuwa alikuwa miongoni mwa mahabusu wengine watano ambao waliuzika mwili wa marehemu Kimathi katika kingo za Mto wa Kamiti.

“Kimathi alinyongwa majira ya asubuhi ya Februari 18, 1957 baada ya kuhukumiwa na jaji Mkuu wa Kikoloni Kenneth O’Connor kwa madai ya kupatikana na silaha na pia kuendeleza vita dhidi ya serikali ya kikoloni,” asema ili kudhihirisha kuwa sio wimbo ambao huwa aliusikia ukiimbwa, bali anaelewa hali na mazingara ya mauti ya Kimathi.

Yeye hufichua kuwa Kimathi alisalitiwa na kundi la wapiganaji lililokuwa linamuunga mkono Mzee Jomo Kenyatta kutwaa urais.

Usaliti

“Marehemu Kimathi alisalitiwa hadi kukamatwa akiwa katika misitu ya Kaunti ya Nyeri ambapo alikuwa ameenda kutembelea mwanamke aliyekuwa na mapenzi naye,” akasema.

Alisema kuwa mabaki ya shujaa huyo yalizikwa mita nne tu katika kingo za mto wa Kamiti.

“Mimi ninaweza kukumbuka ni wapi kwani nilikuwa mmoja wa waliomzika,” akasema.

Mzee huyo alisema kuwa amekuwa akijaribu kutafuta jinsi ya kuwasiliana na serikali katika jitihada za kuyafukua mabaki ya Kimathi na kuyazika kwa hadhi inayomfaa kama mkombozi wa nchi ya Kenya.

“Nimekuwa nikisikia kwa redio eti Kimathi alizikwa katika kaburi la umma katika makaburi ya Lang’ata. Huo ni uongo. Alizikwa kama gaidi wa kawaida kingoni mwa mto,” akasema.

Mzee Maraga alisema kuwa yeye alikuwa mmoja wa mahabusu katika jela hilo wakati walifurushwa kutoka seli zao na kusurutishwa na askari gereza wa kikoloni kwenda kutekeleza mazishi hayo.

Ni hivi majuzi tu Wakili Paul Muite alinukuliwa akisema utafiti wake umeonyesha kuwa mabaki ya Kimathi hayakuzikwa, mbali yalichomwa ama yakaangamizwa kwa kemikali na wakoloni hivyo basi kuondoa matumaini ya kuwahi kupewa mazishi ya kitaifa.

Kusaka mabaki

Hayo yakijiri, nayo serikali ya Argentina imejitolea kusaidia familia ya Kimathi kusaka mabaki yake.

Hayo yalitangazwa na binti wa shujaa huyo, Evelyn Wanjugu akiitaka serikali ya Rais Uhuru Kenyatta iwatimizie ndoto yao kuu ya kuwahi kumpa baba yao mazishi katika shamba lake, Kaunti ya Nyeri.

Kupitia taarifa ya pamoja pamoja na msimamizi wa utafiti wa kimakavazi wa Argentina, Stefan Yauhar,

familia hiyo inasema kuwa inahitaji tu kuonyeshwa mahali alikozikwa ili safari ya mazishi hayo ya heshima ianze.

“Tunahitaji mtu wa kutuongoza katika harakati hizo za kusaka mabaki hayo ambayo hadi sasa haijulikani waziwazi yalikozikwa. Pili, tunahitaji idhini ya serikali ya kutekeleza harakati hizo,” akasema.

Taarifa hiyo ilisema kuwa taifa la Argentina kupitia idara hiyo ya utafiti itahitaji tu kuelekezwa kunakodhaniwa mabaki hayo yanaweza kuwa yamezikwa ili itekeleze uchambuzi wake wa kimaabara.

“Kwa sasa shughuli hiyo itakuwa rahisi kwa kuwa watoto wake wako hai na tunaweza kulinganisha chembechembe muhimu kutoka mabaki hayo na zile za wanawe na hatimaye tuupate ukweli kuyahusu,” taarifa ikasema.

You can share this post!

Uvuvi karibu na Somalia wapigwa marufuku

Serikali yatakiwa kusaka mabaki ya Kimathi, Samoei na Menza

adminleo