• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mpasuko OKA ANC ikitishia kujiondoa

Mpasuko OKA ANC ikitishia kujiondoa

Na CHARLES WASONGA

MPASUKO ndani ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) uliendelea kudhihirika Jumapili siku moja baada ya chama cha ANC kutisha kujiondoa kutoka muungano huo.

Mnamo Jumamosi Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wabunge Tindi Mwale (Butere) na Titus Khamala (Lurambi) walitisha kuwa ikiwa OKA haitamtaja mgombeaji wake wa urais kufikia Desemba 25, 2021, ANC itajiondoa kutoka muungano huo.

Jumapili, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi alikosa kuandamana na vinara wenzake; Kalonzo Musyoka (Wiper) na Gideon Moi (Kanu) katika ibada ya Jumapili na hatimaye mkutano wa hadhara katika eneo la Kiseria, Kajiado.

Badala yake, makamu huyo wa rais wa zamani alihudhuria ibada katika kanisa la Friends Quakers lililoko kando ya barabara ya Ngong, Nairobi.

Naye kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula hakuandamana na wenzake katika maeneo hayo mawili.

Awali, naibu kiongozi wa chama hicho Ayub Savula aliwaambia wanahabari kuwa chama hicho hakikuwa na habari kwamba vinara wenza katika OKA walikuwa wamepanga kuhudhuria ibada katika kaunti ya Kajiado.

“Kiongozi wetu, Musalia Mudavadi amepanga kuhudhuria ibada katika kanisa la Friends Quaker Nairobi. Hana habari kwamba wenzake wameamua kuhudhuria ibada katika Kanisa la kianglikana, Kiserian, Ngong,” Bw Savula ambaye ni mbunge wa Lugari akasema.

Naye Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alisema hivi: “Shughuli ya muungano wa OKA inayojulikana leo (jana Jumapili) na uitakayohudhuriwa na vinara wetu ni ile ya Kajiado. Hatuna habari kuhusu shughuli nyingine.”

Wakihutubia mkutano wa kisiasa baada ya kuhudhuria ibada Kajiado, Seneta Moi na Bw Musyoka walivumisha sera wa muungano wa OKA bila kuwasilisha “salama” kutoka kwa Mbw Mudavadi na Wetang’ula .

Majuma mawili yaliyopita, vinara hao wanne walikuwa pamoja katika ziara ya kuvumisha OKA katika kaunti za Vihiga na Kiambu kabla ya kuhudhuria ibada katika eneo la Makongeni, Thika.

Mnamo Jumamosi, Mbw Malala, Mwale na Khamala, waliokuwa wakituhubu eneo la Matunda, Kaunti ya Kakamega, walisisitiza kuwa mgombeaji wa urais atakayeteuliwa na OKA sharti awe kiongozi wao, Bw Mudavadi.

Watatu hao walitisha kuwa ikiwa OKA haitamtaja kiongozi wao kuwa mgombeaji urais ANC itajiondoa na “kushirikiana na marafiki wengine katika safari ya kuelekea Ikulu.”

“Tunawaambia wenzetu katika OKA kwamba tunataka kujua mgombeaji urais wa muungano huo kabla ya Desemba 25. Ikiwa mgombeaji huyo, ambaye tunajua ni Musalia Mudavadi, hatatajwa basi sisi kama ANC tutaondoka ili tuunde muungano mwingine utakaomwezesha Musalia kupata urais,” Bw Mwale akasema.

Huku akiunga mkono kauli ya Mwale, Khamala aliielezea imani kwamba Bw Mudavadi ataibuka mshindi ikiwa atapewa tiketi ya urais ya OKA.

“Hatuamini kuwa OKA itashindwa katika uchaguzi mkuu ujao ikiwa itamteua Musalia Mudavadi kuwa mgombeaji wake wa urais. Hii ndio maana tunataka kujua mgombeaji wetu wa urais haraka iwezekanavyo,” akasema Khamala.

Naye Seneta Malala alisema, Wakenya wana hamu ya kujua mgombeaji urais wa OKA kwa “muda unayoyoma”

“Kando na mgombeaji urais, Wakenya wanataka kujua nani atakuwa mgombeaji mwenza wa OKA ili waweze kufanya uamuzi bora debeni mwaka 2022,” akaeleza. 

You can share this post!

Scotland wapepeta Moldova na kufuzu kwa mchujo wa kuwania...

TAHARIRI: Serikali iepuke mvutano na Miguna Miguna

T L