• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Ataka mkataba kati ya viongozi Mlimani na wawaniaji Urais

Ataka mkataba kati ya viongozi Mlimani na wawaniaji Urais

Na CHARLES WANYORO

ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, amewataka viongozi waliochaguliwa kutoka ukanda wa Mlima Kenya kutia saini mikataba ya kabla ya uchaguzi na wawaniaji mbalimbali wa kiti cha Urais kuelekea uchaguzi 2022.

Kwa mujibu wa Bw Kiunjuri, mikataba hiyo itatoa ufafanuzi jinsi ambavyo watanufaika serikalini iwapo mwaniaji wanayempigia debe atafanikiwa kushinda kiti cha urais.

Kiongozi huyo wa The Service Party (TSP) alisema kuwa bila mikataba hiyo, huenda eneo la Mlima Kenya linalojivunia wapigakura wengi likaachwa nje ya serikali ijayo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu mwaka 2022.

Hasa alisisitiza kuwa mwaniaji atakayeungwa mkono na wakazi wa mlimani lazima aahidi kuwa atatenga mgao zaidi ya fedha kwa kaunti zote za eneo hilo.

Bw Kiunjuri alisisitiza kura ya maamuzi lazima ifanyike siku 100 baada ya uchaguzi ujao na kiongozi atakayeshabikiwa lazima atimize hilo kama njia ya kuongezea Mlima Kenya maeneobunge zaidi pamoja na rasilimali nyinginezo zinazohitajika.

Aidha alionya wakazi wa mlimani kuhadaiwa na wadhifa wa Naibu Rais ilhali tatizo lao ni uwakilishi huku maeneo mengine yakionekana kunufaika kuwaliko licha ya idadi yao kubwa.

“Badala ya kukimbia kuwapigia debe wawaniaji mbalimbali wa kiti cha urais, lazima tuulize kwanza jinsi watu wetu watakavyonufaika. Je wakulima wetu watanufaika kivipi na watatuongezea rasilimali? Hakuna eneo ambalo limehiniwa kimapato kama mlimani ambalo lina idadi kubwa ya raia,” akasema.

Mbunge huyo wa zamani wa Laikipia Mashariki alisema kuwa asilimia 80 ya yale yaliyokuwa katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) iliyotupiliwa mbali na korti yalikuwa mazuri na ni vyema iwapo yatatekelezwa na serikali inayokuja.

Ripoti hiyo hasa ilimakinikia uwakilishi sawa na mgao sawa wa rasilimali za kitaifa.

Bw Kiunjuri ambaye anadaiwa sasa analenga kiti cha eneobunge la Laikipia Mashariki, alitoa wito kwa serikali ihakikishe kuwa kuna usalama katika kaunti hiyo na maeneo mengine ya Bonde la Ufa.

Kulingana naye kila mara machafuko yanapotokea, watu wanaoumia ni watu kutoka Mlima Kenya.Bw Kiunjuri hivi majuzi aliingia kwenye muungano wa kisiasa na kinara wa Narc-Kenya Martha Karua na mbunge wa Gatundu Moses Kuria.

Alisema jambo la muhimu hasa ni jinsi ambavyo, wale wanaosaka kura za Mlima Kenya watawasaidia wakazi wala si hadaa tupu kuwa watapokezwa nafasi ya Naibu Rais.

You can share this post!

USWAHILINI: Posa asili ya Kidigo ilivyofanikishwa kwa...

WASONGA: Vinara wa OKA wanawakanganya wafuasi wao

T L