• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
WASONGA: Vinara wa OKA wanawakanganya wafuasi wao

WASONGA: Vinara wa OKA wanawakanganya wafuasi wao

Na CHARLES WASONGA

VINARA wa One Kenya Alliance wanafaa kukataa kushiriki mikutano na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu na waendelee na kampeni za kuuza sera zao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Ni unafiki mkubwa kwa wanasiasa hao kulalamika hadharani kila mara kwamba Rais Kenyatta anawashinikiza kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga na kwa upande mwingi ni wepesi kuitikia mialiko ya Rais Ikulu kujadili ajenda hiyo hiyo.

Kwa mfano, mnamo Jumamosi wanasiasa hawa, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) walihiari kusitisha kampeni ambazo walikuwa wameratibu katika Kaunti ya Vihiga na kuelekea Ikulu ya Nairobi.

Kwa kuitikia mialiko ya Rais Kenyatta kila mara anapowaita, wanne hawa wamejitokeza kama wanasiasa wasio na misimamo thabiti.

Kwa kiwango fulani wanaonekana kama wanasiasa ambao hawana uhakika kama watadhamini mmoja wao kuwania urais 2022 au wataungana na mrengo wa Bw Odinga au ule wa Naibu Rais William Ruto.

Wanawakanganya wafuasi wao, na Wakenya kwa ujumla, kila mara wanafululiza katika Ikulu na baadaye wanatumia muda mwingi kulalamika kwamba Rais anawalazimisha kuunga mkono Bw Odinga.

Nadhani wafuasi wao watawaamini zaidi ikiwa watakataa kwenda kujadili suala hilo na watumie muda wakati wao kuuza sera za OKA katika pembe zote za nchini.

Wanasiasa hawa wakumbuke kwamba vinara wa uliokuwa muungano wa NARC walikubalika zaidi na Wakenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2002 kwa sababu hawakuwahi kukataa katakata kuunga mkono Rais Kenyatta ambaye alikuwa chaguo la Rais wa zamani marehemu Daniel Moi.

Vinara hao Narc wakiongozwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki na Bw Odinga, hawakuwahi kuitikia mialiko ya kuhudhuria mikutano Ikulu kujadili siasa za urithi.

Walitumia muda wao mwingi kuuza sera zao kote nchini hata baada ya Bw Kibaki kupata ajali na kupelekwa ng’ambo kwa matibabu.

Hii ilichangia Wakenya kuwaamini vinara wa Narc na hatimaye Bw Kibaki aliibuka mshindi katika uchaguzi wa urais licha ya kwamba Rais Kenyatta aliungwa mkono na asasi zote za serikali.

Kwa hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa vinara wa OKA wakutabaliane kuhusu ni nani atapeperusha bendera ya urais chini ya mwavuli wa muungano huo ili Wakenya wajue kwamba kutakuwepo na mirengo mitatu katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Ilivyo sasa kati ya vinara hao wanne, ni Bw Wetang’ula pekee ambaye hajatangaza nia yake ya kuwania urais.

Mbw Mudavadi, Musyoka na Gideon tayari wamekwisha kutangaza kuwa watawania urais ambapo wanatarajiwa kushindania tiketi ya OKA.

Kwa hivyo, wateue mmoja wa hawa watatu ili waanze kumuuza kwa Wakenya.

Wakome kabisa kukutana na Rais Kenyatta ambaye tayari inaonekana ameamua chaguo lake ni Bw Odinga.

You can share this post!

Ataka mkataba kati ya viongozi Mlimani na wawaniaji Urais

NGILA: Jina jipya la Facebook liambatane na maadili

T L