• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Azimio wamtaka Ruto atimize ahadi zake kwa Wakenya

Azimio wamtaka Ruto atimize ahadi zake kwa Wakenya

NA DAVID MWERE

KUNDI la wabunge kutoka muungano wa Azimio limemkumbusha Rais Mteule William Ruto kuwa wakati umewadia wa kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni anapokula kiapo hii leo lakini wakamwonya dhidi ya kuingilia Mtaala Mpya wa Elimu (CBC).

Wabunge hao Bw Opiyo Wandayi (Ugunja) na Bw Jared Okelo (Nyando) waliwaongoza wabunge wenzao wenye mtazamo sawa walizungumza Jumanne kwenye majengo ya bunge ambapo walimkosoa Rais Mteule kwa kuanza vibaya kwa kuvutia upande wake wabunge wa vyama pinzani.

Aidha, walikashifu suala la ukabila “linalochochewa na watu walio karibu na Rais Mteule” kupitia mafumbo na jumbe kwenye mitandao ya kijamii.

“Wakenya wanaumia. Bei ya Unga, gesi ya kupikia, nauli, kodi ya nyumba, bidhaa za petroli miongoni mwa mengine, yanawatesa watu wetu. Tunatarajia suluhisho la dharura ili Wakenya wasiendelee kuteseka zaidi pindi utakapochukua afisi,” alisema Bw Wandayi.

Hata hivyo, wabunge hao walifafanua kuwa hawazungumzi kwa niaba ya muungano wa Azimio, ambao kiongozi wa chama chao cha ODM Raila Odinga alitumia kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wakati wa kampeni, Rais Mteule aliahidi kupunguza gharama ya maisha miongoni mwa mengine, atakapoapishwa rasmi.

Waliapa kuwa juhudi za rais mteule za kuwanunua viongozi na vyama vya kisiasa na kuvijumuisha ndani ya UDA hakutaua maoni yao mbalimbali.

Walisema kuwa “kama taifa tumesafiri mwendo mrefu hatuwezi kurudi nyuma.”

“Ni mkondo tunaofahamu uliosababisha Kenya kuwa taifa la chama kimoja hali ambayo ilichukua miaka mingi iliyojaa uchungu na kujitolea mhanga kubadilisha. Uamuzi ni wake vilevile.”

“Lakini Bw Ruto ni sharti afahamishwe mambo mawili kuwa anaweza akawanunua viongozi binafsi lakini sio taifa lote. Anaweza kujaribu kurejesha Kenya kuwa nchi ya chama kimoja, lakini ataanguka sawa na jinsi watangulizi wake walivyofanya. Wakenya hawatamruhusu.”

Wabunge hao walisisitiza kuwa matarajio yao ni kwamba Rais Mteule ataelewa kuwa kuna mtanziko kati ya furaha ya wafuasi wake na hofu kwa walke ambao hawakumpigia kura na wanaamini hakushinda.

“Hususan, kuna hofu kuhusu wingu na roho ya kisasi ambayo imegubika kampeni ya Ruto na inavuja kutoka kwa wandani wake. Tunasema uamuzi ni wa Ruto,” alisema Mbunge wa Ugunja.

Wasiwasi kuhusu mfumo wa elimu nchini ulitajwa vilevile huku wabunge hao wakitahadharisha serikali ya Ruto dhidi ya kufutilia mbali CBC.

Wakati wa msimu wa kampeni, Bw Ruto aliahidi kupiga teke CBC, katika mwaka wake wa sita na ambayo kufikia sasa imemeza mabilioni ya pesa za walipa ushuru na ufadhili wa wahisani kwenye juhudi za kujenga miundomsingi inayohitajika na gharama ya mafunzo.

  • Tags

You can share this post!

Ruto achagua kijani kibichi kama rangi rasmi ya bendera...

Marais na viongozi wanaotarajiwa kushuhudia Dkt Ruto...

T L