• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Ruto achagua kijani kibichi kama rangi rasmi ya bendera yake ya urais

Ruto achagua kijani kibichi kama rangi rasmi ya bendera yake ya urais

NA MARY WAMBUI

RAIS mteule Wiliam Ruto amechagua rangi ya kijani kibichi ya bendera yake ya urais ambayo itakuwa ikipeperushwa kila mahali atakapokuwa baada ya kuapishwa leo Jumanne.

Kila rais huwa na bendera yake rasmi, inayopeperushwa kando ya bendera ya taifa popote rais anakoenda na inashukiwa punde tu akiondoka.

Inaundwa na kutengenezwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) anavyopenda Rais mteule.

Maelezo kuhusu alama nyingine ambazo zitakuwa katika bendera hiyo hata hivyo hayakufichuliwa. Hata hivyo, itakuwa na mikuki miwili iliyopitana na ngao zilizo na rangi za bendera ya taifa.

Hizi mbili zinaashiria umoja na kuwa tayari kulinda uhuru wa nchi.

“Tunataka siri kidogo. Tusubiri Rais wa Tano aje na kuvunua bendera yake hapa. Sijui kama anataka itajwe leo,” alisema Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho alipotoa taarifa kuhusu mipango uapisho Jumanne.

Iwapo Dkt Ruto atafuata utaratibu wa kuunda bendera za marais wa waliotangulia, bendera yake itakuwa na alama ya chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) ya wilibaro ambayo kulingana na tovuti ya chama hicho inaashiria “thamani, utu na heshima ya kazi kwa kujenga jamii yenye usawa”.

Rais Uhuru Kenyatta alichagua bendera inayofanana na iliyokuwa ya baba yake, hayati Mzee Jomo Kenyatta, ya rangi ya bluu.

Hata hivyo aliongeza alama ya njiwa ya chama cha The National Alliance (TNA) kinyume na ya baba yake iliyokuwa na alama ya jogoo ya chama cha Kenya African National Union (KANU).

Rais Moi alichagua bendera ya rangi ya kijani kibichi ikiwa na alama ya jogoo naye Rais Mwai Kibaki akachagua ya yangi nyeupe iliyokuwa na matawi ya mzeituni.

  • Tags

You can share this post!

Ruto kurithi zigo la utawala wa Uhuru

Azimio wamtaka Ruto atimize ahadi zake kwa Wakenya

T L