• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Azimio yavuna Mlimani Kiraitu akitangaza kumuunga Raila

Azimio yavuna Mlimani Kiraitu akitangaza kumuunga Raila

NA GITONGA MARETE

MUUNGANO wa Azimio la Umoja ulivuna pakubwa Jumatano, baada ya Gavana wa Meru Kiraitu Murungi kutangaza kwamba atamuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwania urais mnamo Agosti.

Bw Murungi aliwaongoza zaidi ya wajumbe 500 wa chama chake cha Devolution Empowerment Party (DEP) kujiunga na vuguvugu hilo, hivyo kuondoa matumaini ya chama hicho kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Kwenye ziara aliyofanya majuzi katika Kaunti ya Meru, Naibu Rais William Ruto alimrai Bw Murungi kujiunga na kambi yake ya kisiasa

Hata hivyo, gavana huyo alisema atamfanyia kampeni Bw Odinga ili kuhakikisha amezoa kura nyingi katika eneo hilo.

“Nimeangalia na kutathmini kwa kina wawaniaji wote wa urais. Baada ya tathmini hiyo, nimefikia uamuzi kwamba Bw Odinga ndiye kiongozi pekee anayeweza kuistawisha nchi hii. Amejitolea kupigania demokrasia na ugatuzi. Ninaamini ndiye atakuwa rais wa tano wa Kenya,” akasema Bw Murungi, alipowahutubia wajumbe hao katika Kanisa la St Michael, mjini Meru.

Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, aliye pia mwenyekiti wa Bodi ya Kampeni za Bw Odinga, alisifia uamuzi wa Bw Murungi, akisema hatua hiyo itampiga jeki sana Bw Odinga kisiasa katika eneo hilo.

“Huu ni wakati wa Bw Odinga. Tuna furaha kuwa Bw Murungi amefanya uamuzi ufaao,” akasema, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Bw Murungi anatarajiwa kujiunga na Waziri wa Kilimo Peter Munya na mbunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini) kumfanyia kampeni Bw Odinga katika eneo hilo. Bw Maore ndiye Naibu Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Kwenye Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC), Jumanne, wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuunga mkono vuguvugu hilo.

Kwa miezi kadhaa iliyopita, Bw Murungi amekuwa akisubiriwa kuamua iwapo atamuunga mkono Bw Odinga au Dkt Ruto.

Gavana huyo alitoa tangazo hilo baada ya Seneta Mithika Linturi kutangaza kuwa atawania ugavana kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto.

You can share this post!

Anayedaiwa kubaka na kuiba apewa dhamana

Mshukiwa ambaye alichomoa pingu na kuhepa polisi asakwa

T L