• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
CHARLES WASONGA: Matokeo ya Msambweni yasihusishwe na BBI wala kura za 2022

CHARLES WASONGA: Matokeo ya Msambweni yasihusishwe na BBI wala kura za 2022

Na CHARLES WASONGA

KWA mujibu wa kipengele cha 38 (2) cha Katiba ya sasa, ni haki ya kila Mkenya kufanya maamuzi yake ya kisiasa kwa kuchagua watu anaotaka wamwakilishe katika asasi mbalimbali za uongozi wa nchini.

Mojawapo ya asasi hizo ni bunge la kitaifa ambalo lina wajibu wa kutunga sheria, kuhakiki utendakazi wa serikali kuu na kusikiza malalamishi kutoka kwa raia kupitia wabunge.

Baada ya kila uchaguzi, wapiga kura katika eneo fulani la uwakilishi huwa na wingi wa matumaini kwamba waliyemchagua atafanyia kazi kulingana na wajibu wa afisi hiyo.

Chini ya kivuli hiki, ninaamini kuwa asilimia 38 ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi mdogo wa katika eneo bunge la Msambweni walimchagua Feisal Bader baada ya kushawishika kwamba ndiye anayeweza kushughulikia ipasavyo matatizo yao.

Sidhani kwamba wapiga kura wote 15,251 waliojitokeza kumpigia kuwa mwanasiasa huyo aliyewania kiti hicho kama mgombea huru walifanya hivyo kwa misingi ya ushawishi kutoka kwa Naibu Rais William Ruto, Gavana wa Kwale Salim Mvurya na wanasiasa wengine wa mrengo wa Tangatanga waliopiga kambi katika eneo hilo.

Yapasa ieleweke kuna sababu zingine zenye uzito zaidi zilizowavutia wapiga kura kumchagua Bw Bader. Kwa mfano, huyo ni mtu ambaye amewahi kufanyakazi na mbunge wa zamani Suleiman Dori kama msimamazi wa Hazina ya Ustawi wa Eneo bunge (CDF) hilo kwa zaidi ya miaka minane.

Hii ni kando na kwamba marehemu Dori ni mjombake.Bila shaka hii ilimfaidi kisiasa Bw Bader kwani wapiga kura wengi walimwona kama mtu ambaye amekuwa akiwahudumia akisimamia miradi mipango ya CDF kama vile utoaji fedha za misaada ya masomo (basari) kwa watoto wao.

Waama, Waswahili husema; Usiache mbachao kwa msala upitao.Kwa hivyo, tofauti na wagombea wengine akiwemo Omar Boga wa ODM, Bw Bader alikuwa katika nafasi bora ya kutwaa kiti hicho kwa urahisi kwa sababu ni mtu ambaye utendakazi wake umeonekana kupitia nafasi aliyoshilikia kama msaidizi wa Dori.

Pili, hatua ya Gavana wa Kwale Salim Mvurya kumpigia debe Bw Bader alimsaidia zaidi kupata uungwaji mkono kutoka kwa wengi wapiga kura wa Msambweni.

Kwa nini?

Gavana Mvurya anayehudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, ana ushawishi mkubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kwa sababu amefanya kazi nzuri tangu alipochaguliwa mnamo 2013 na anatoka kabila la walio wengi la Waduruma.

Kwa hivyo, mchango wa mawimbi ya siasa za Tangatanga, Kieleweka, ODM au mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI ulikuwa finyu zaidi katika kuamua mshindi wa kinyang’anyiro hicho.

Ndiposa ilikuwa makosa kwa Bw Odinga kunasibisha matokeo ya uchaguzi huo na umaarufu wa BBI katika eneo hilo.

Vile vile, ni makosa kwa wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga kuwahadaa Wakenya kwamba matokeo ya uchaguzi huo mdogo yanaashiria kuwa Wakenya wamekataa mageuzi ya Katiba kupitia BBI, handisheki au eti yanaonyesha kuwa Dkt Ruto atashinda katika uchaguzi mkuu wa 2022.

[email protected]

You can share this post!

Matiang’i aagiza machifu kusaka wanafunzi watakaokaidi...

WANDERI KAMAU: Ulaya irejeshe mali ya Afrika ambayo...