• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
DEMOKRASIA: Wamiliki wa tuktuk waifunza IEBC jinsi ya kusimamia uchaguzi

DEMOKRASIA: Wamiliki wa tuktuk waifunza IEBC jinsi ya kusimamia uchaguzi

Na SAMMY WAWERU

KATIKA kila mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Kenya, tumeshuhudia mizozo ya hapa na pale huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikinyooshewa kidole cha lawama na vyama vya kisiasa, mashirika ya kijamii na wananchi kwa jumla. 

Mivutano hutokea mirengo pinzani ikituhumiana kwa kuboronga mchakato mzima nzima wa upigaji kura na matokeo, kwa pupa za kutaka kukwamilia mamlaka.

Kilele cha majibizano kati ya mafahali wakuu huwa vurugu, ghasia, mauaji na watu kufurushwa makwao kila baada ya miaka mitano.

Wapigakura kwenye foleni kuchagua viongozi wapya wa Muungano wa Wamiliki wa Tuktuk mtaani Githurai (GTA) mnamo Februari 8, 2019. Picha/ Sammy Waweru

Taswira ya chaguzi kuu huwa sawa na za mchujo, za baadhi ya vyama vya ushirika, viwanda, na wagombea waliobwagwa kwa nyadhifa mbalimbali hulalamikia kuibiwa kura. Hii ni nchi inayothamini demokrasia, na matukio ya aina hiyo yanaikandamiza.

Hata hivyo, kundi moja la wamiliki na wahudumu wa tuktuk mtaani Githurai 45, Kaunti ya Kiambu limedhihirisha migogoro katika uchaguzi inaweza kuepukika endapo wahusika watashirikiana kwa maandalizi bora na shughuli ya kuchagua viongozi iwe ya huru, haki na wazi.

Muungano wa Wamiliki wa Tuktuk mtaani Githurai (GTA) mnamo Ijumaa Februari 8, ulifanya uchaguzi wake wa viongozi, wa mwaka huu ukiwa wa nne. Uchaguzi wake hufanywa kila mwaka.

Ndoo za plastiki zilizotumiwa kupigia kura. Picha/ Sammy Waweru

Kinyume na chaguzi za awali zilizoshuhudia kizaazaa, uchaguzi wa mwaka huu ulitajwa kama komavu na ulioonesha ukuaji wa demokrasia.

“Katika historia ya GTA hatujawahi shuhudia uchaguzi wenye amani kama huu,” alisema mkuu wa kaunti ndogo ya Ruiru (awali cheo hiki kikijulikana kama D.O) Bw Peter Kimeu.

Sawa na maandalizi ya tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini (IEBC), uchaguzi wa GTA 2019 ulikuwa na karatasi za kupiga kura zilizochapishwa majina ya wagombea wa nyadhifa mbalimbali.

Wapigakura wasubiri matokeo. Picha/ Sammy Waweru

Nyadhifa zilizowaniwa zilikuwa saba; Mwenyekiti, naibu mwenyekiti, katibu mkuu, naibu katibu mkuu, katibu mshirikishi, mweka hazina na mkuu wa nidhamu.

Masanduku ya kura yaliandikwa majina ya kila wadhifa. Sajili ya kupiga kura iliandaliwa na walioshiriki ni wamiliki wa tuktuk na madereva wao, ambapo kila mmoja alitakiwa kuandikisha jina lake alipowasili kisha linathibitishwa kwa mujibu wa sajili.

Vifaa vya kupiga kura vilihifadhiwa katika ofisi ya mkuu wa kaunti ndogo ya Ruiru iliyoko wadi ya Mwiki, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi wa utawala (AP).

Mpigakura akichagua viongozi.P icha/ Sammy Waweru

Kituo cha kupiga kura (ukumbi wa mikutano wa wadi ya Mwiki) kilipofunguliwa rasmi mwendo wa saa nne asubuhi, karatasi za kura na masanduku zilisafirishwa zikilindwa na maafisa wa AP chini ya Inspekta Thiong’o na Sajenti Kandie.

Walioruhusiwa kuwa kituoni ni maajenti, karani na makamishna wa muda walioteuliwa kuusimamia. Wapiga kura walitakiwa kuwa nje ya mazingira ya kituo, ambapo walipiga foleni na baada ya kupewa pasi maalumu yenye nambari na jina la mshiriki kupigwa mstari sajilini aliingia.

Aidha, karani alimkabidhi karatasi za kura, akikamilisha kuchagua kiongozi aliyetaka alitia kila kura kwa sanduku lake.

Wapigakura wachukua muda kuteua viongozi wanaotaka. Picha/ Sammy Waweru

Mkondo wa IEBC kupaka kidole rangi kwa waliopiga kura uliigwa katika uchaguzi wa GTA ili kuepuka utovu wa nidhamu, kwa kushiriki zaidi ya mara moja.

Kwa waliopiga kura, kituoni na mazingira yake ilikuwa marufuku. Shughuli hizo zilikamilika saa sita na nusu, zoezi la kuhesabu likaanza na walioshiriki waliruhusiwa kuingia ili kufuatilia kwa karibu.

Walioibuka kidedea walitangazwa rasmi na mmoja wa afisa msajili wa vyama vya ushirika eneobunge la Ruiru. Bw Peter Kinyua almaarufu Energy ndiye alichaguliwa kama mwenyekiti wa GTA, naibu wake akiwa Laban Gitonga.

Baad ay kupiga kura, kila mpigakura hutiwa alama ya wino kuonyesha ameshashiriki kwa mchakato huo asije kupiga kura tena. Picha/ Sammy Waweru

Kinyua alizoa kura 223 dhidi ya mpinzani wake aliyetambulika kama Wa Kamau ambaye alipata kura 50. Wapiga kura 273 ndio walishiriki shughuli hiyo.

Mwenyekiti mteule alihimiza wahudumu na madereva kushirikiana ili kuimarisha biashara ya tuktuk Githurai 45.

“Ninawapongeza walionichagua na hata wale ambao hawakunipa kura, nitakuwa kiongozi wa wote. Tushirikiane ili kustawisha uwekezaji wa tuktuk,” alisema Bw Kinyua.

Mwenyekiti anayeondoka, James Nyaga aliahidi kuunga mkono afisi iliyochaguliwa akiwashauri kustahimili changamoto zinazokumba viongozi.

Baadhi ya viongozi wa GTA waliochaguliwa, mwenyekiti Bw Peter Kinuyua akifuatwa na naibu wake Labana Gitonga (wenye shati za samawati) . Picha/ Sammy Waweru

“Kwa hakika uongozi si jambo rahisi, ninashukuru kwa muda niliokuwa mamlakani. Langu ni kuwatakia kila la heri, mkihitaji usaidizi niko radhi kuwaelekeza,” alisema.

Huduma za tuktuk Githurai 45 zilianzishwa mwaka wa 2014, na ndipo GTA ilibuniwa. Muungano huo una zaidi ya vijigari 300.

Denson Machuki, mchanganuzi wa masuala ya uongozi anasema ukomavu ulioonyeshwa na GTA unapaswa kuigwa na kampuni na mashirika, yasiyokosa mizozo wakati wa chaguzi za viongozi wake.

Anaeleza kwamba ukuaji wa demokrasia katika taifa linalodai kuwa na uhuru unapimwa kupitia shughuli kama hiyo, ambayo ikikosa kudhibitiwa inaathiri uchaguzi mkuu.

“Kinachosababisha migawanyiko wakati wa uchaguzi ni ubinafsi, siasa za ukabila na tamaa ya viongozi kutaka kuwa mamlakani ili kujinufaisha. Wananchi wawe makini kwa viongizi kama hao, wawaangushe debeni” asema Bw Machuki.

You can share this post!

Mema Foundation Academy inavyonoa vipaji vya soka licha ya...

Kimani Ngunjiri amkejeli gavana kwa kutelekeza watoto

adminleo