• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Dkt Mutua awataka wanasiasa kuheshimu familia za waliofiwa

Dkt Mutua awataka wanasiasa kuheshimu familia za waliofiwa

Na SAMMY WAWERU

Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua amewakashifu vikali viongozi na wanasiasa wanaoendesha siasa katika hafla za mazishi.

Dkt Mutua amesema hatua hiyo ni kukosea heshima familia na jamaa zilizofiwa, wakati ambapo wanaomboleza.

Akitumia mfano wa hafla ya mazishi ya Seneta wa Machakos Boniface Kabaka mnamo Desemba 22, 2020, kiongozi huyo wa Maendeleo Chap Chap alisema ilikuwa taswira ya aibu wanasiasa waliokuwepo baada ya kutoa salamu za pole alizosema zilisheheni siasa tupu, wengi waliondoka hata kabla mwili wa marehemu haujazikwa.

“Kulikuwa na wanasiasa na viongozi wengi, wakiwemo wabunge na maseneta. Baada ya kupiga siasa, wote waliingia kwenye ndege wakaondoka, hakukuwa na wa kusaidia kupeleka jeneza la marehemu kaburini (akimaanisha maseneta kumpa mwendazake heshima za mwisho),” Gavana akasema.

Alisema ilikuwa picha ya aibu, ikizingatiwa kuwa walitumia jukwaa la mazishi ya Seneta Kabaka kufanya kampeni, bila hata kuheshimu familia yake iliokuwa ikiomboleza kumpoteza mpendwa wao.

“Ni aibu, tabia mbaya kufanya siasa kwenye mazishi. Ikiwa mtu anataka kufanya siasa aandae hafla za hadhara ila si kwa mazishi,” Dkt Mutua akasema.

Kauli ya gavana imejiri siku chache baada ya mbunge wa Dagoretti, Bw Simba Arati na mwenzake Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini) kuangushiana makonde katika hafla ya mazishi Kisii.

You can share this post!

Wewe si ‘hasla’, ulikuwa karibu na Mzee Moi...

Mswada wa Kura ya Maamuzi kupewa kipaumbele bungeni