• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Gachagua asema ndiye wa kuaminiwa kutetea maslahi ya Mlima Kenya

Gachagua asema ndiye wa kuaminiwa kutetea maslahi ya Mlima Kenya

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Mteule Rigathi Gachagua Jumatano, Agosti 24, 2022, amesema kuwa yeye ndiye atamrithi Rais Uhuru Kenyatta kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya.

Akiongea katika mkutano wa kampeni katika eneo bunge la Rongai, kaunti ya Nakuru, Bw Gachagua amesema kuwa hakutakuwa na pengo lolote la uongozi katika eneo hilo baada ya Rais Kenyatta kustaafu.

“Watu wamekuwa wakiuliza nani atapigania eneo la Mlima Kenya baada ya Uhuru kustaafu. Ningependa kuwahakikishia kwamba niko hapa, nitawatetea watu wetu,” akasisitiza.

Bw Gachagua amesema hayo alipoongoza kampeni za kumpigia debe mgombeaji ubunge wa Rongai kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Paul Chebor.

Bw Chebor anapambana na mbunge wa eneo hilo Raymond Moi ambaye anatetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha Kanu.

Rongai ni mojawapo ya maeneo wakilishi ambako uchaguzi utafanyika mnamo Jumatatu, Agosti 29, 2022.

Maeneo mengine ambako uchaguzi wa ubunge utafanyika ni; Kacheliba, Pokot Kusini na Kitui Mashambani.

Aidha, uchaguzi wa ugavana utafanyika katika kaunti za Mombasa na Kakamega.

Chaguzi katika maeneo hayo hazikufanyika mnamo Agosti 9, 2022, kutokana na kile Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilidai ni hitilafu katika karatasi za kupigia kura.

Jumatano, Bw Gachagua ameongeza kuwa ataelekeza wakazi wa Mlima Kenya akishirikiana na Rais mteule William Ruto.

Serikali ya Dkt Ruto, akasema, itahakikisha kuwa Rais Kenyatta analipwa malipo yake yote ya kustaafu huku akipewa huduma zote zilizoainishwa kwenye Katiba.

“Kulingana na Katiba, atapokea malipo, magari na wafanyakazi ambao watamhudumia. Hii itakuwa ni sehemu ya manufaa atakayopata baada ya kustaafu,” Gachagua akasema.

  • Tags

You can share this post!

Raila aambiwa mwenyekiti IEBC hasimamii uchaguzi wa ugavana

Jeremiah Kioni adai maajenti wa Azimio walifurushwa Mlima...

T L